Na Khadija Kalili, Michuzi TV
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeanza ziara ya wiki mbili wakifanya uchunguzi wa kero na malalamiko ya wafanyakazi na wakazi wa maeneo jirani ya viwanda vya mkoa wa Pwani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 12 Machi 2025 Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Nyanda Shundi katika ziara hiyo wilayani Kibaha amesema
lengo la ziara hiyo ni kuangalia hali ya haki za binadamu na uzingatiwaji wa misingi ya utawala bora usalama wa mazingira ya kazi na uzingatiwaji wa viwango vya ajira kiwandani hapo.
Kamishna amesema kuwa wamefika hapo na kujionea hali halisi na kusisitiza tume itafanya uchunguzi wake kwa kutumia wakaguzi wao ,kadhalika OSHA watakuja tena kufanya ukaguzi pia tayari walishakuja katika siku za nyuma kulikua na changamoto walizozibaini lakini tayari uongozi umeshazirekebisha baadhi ya chanamoto hizo.
“Tume ni sawa na sikio la Serikali pindi tunapopata malalamiko kutoka kwa wananchi tunanyanyuka ofisini na kwenda kuwatembelea ikiwa ni pamoja na kuongea na pande zote mbili,hadi Tume kufika hapa ieleweke kuwa kuna kitu kimetuleta”
” niseme tu nawashukuru wananchi kwa kutoa taarifa ukiona haki yako inavunjwa au ukaona haki ya mtu mwingine inavunjwa na ukakaa kimya jua kuna siku haki yako itavyunjwa” amesema Kamishna Shuli
Akifafanua kuhusu muda sahihi wa kutatua malalamiko waliyoyapata amesema kuwa kadri uchunguzi unavyoendelea kuna mambo yatajitokeza, mfano hayo maji yanayolalamikiwa na wananchi kwamba yanatiririshwa kutoka Kiwandani itakazimu wataalamu waje wayachukue wakayapime kama kwani wao ndiyo wenye mamlaka ya kutoa majibu sahihi amesema Kamishna Shuli
Aidha amesema kuwa Tume hiyo itaendelea na ziara ya kutembelea viwanda ambavyo wananchi wametoa malalamiko.
Aidha Kamishna ametoa shukran kwa Uongozi wa Kiwanda Cha Keds kwa ushirikiano mkubwa waliowaonesha.
“Tume imeambatana na Taasisi za Serikali ambazo ni OSHA, NEMC na Maafisa kutoka Ofisi ya RAS ,Afisa Biashara, Afisa Kazi na Afisa Maendeleo ya jamii wote kutoka Mkoa wa Pwani huku lengo kubwa likiwa kuleta ufanisi katika ziara hiyo
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Keds Bob Chen amesema kuwa Kiwanda chao ni wazalishaji wa bidhaa za sabuni, taulo za kike na taulo za kike ambazo huuzwa ndani ya nchi na nje ya nchi huku wakizingatia sana usalama wa afya za wafanyakazi pamoja na jamii inayoishi katika maeneo ya jirani ya kiwanda hicho.
“Asilimia 60 ya wafanyakazi wetu wanaishi jirani na Kiwanda hivyo kama kungekua na madhara basi wangeanza kudhurika wao hata kwenye rekodi zetu hatujawahi kupata malalamiko yanamna yoyote” amesema Bob.
Amekanusha kwamba maji yanayotiririka kutoka Kiwandani hayana sumu kwani malighafi kuu ni mchanga na laiti kama yangekuwa na sumu basi wafanyakazi wao ambao wanashinda na kukesha kiwandani wangeshapata madhara.
Meneja wa Keds Tanzania Limited Michael Lugalela amesema kuwa kiwanda hicho kimejengwa kwa dhamira njema na lengo kubwa kukuza uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa Mkoa na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla .