OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa maelekezo mahsusi nane kwa viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwamo kufanya tathmini ya kina na kuchukua hatua za haraka kwa watumishi wanaoshiriki kuhujumu mfumo wa mapato kwenye maeneo yao.
Akifunga Machi 12, 2025 Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri Mchengerwa, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. DFesto Dugange, amewataka wafanye tathmini hiyo ili kuhakikisha hakuna upotevu au uvujaji wa mapato mikononi mwa watumishi.
Aidha, ameelekeza kupatiwa taarifa ya namna kila Halmashauri zilivyokusanya katika vyanzo kodi ya majengo, ushuru wa mabango na kodi ya Ardhi ili ili kupima ufanisi.
Pia, ameagiza Halmashauri zisimamie kikamilifu utoaji wa huduma bora za afya ili kuondoa malalamiko ya wananchi kwa serikali na ziweke mikakati madhubuti ya kudhibiti upotevu wa fedha za uchangiaji wa huduma za afya.
Kuhusu elimu, ameelekeza wahakikishe wanasimamia uandikishaji wa madarasa ya awali, darasa la kwanza na makundi mengine kutokana na hali kutoridhisha kwa baadhi ya mikoa sambamba na kuthibiti mdondoko wa wanafunzi.
Mhe. Waziri Pia ameelekeza Halmashauri zinazotekeleza miradi ya TACTIC ambayo Wakurugenzi wamesaini mikataba, hakikisheni wanasimamia utekelezaji kwa viwango, ukubwa wa kazi, muda unaotakiwa na fedha itumike kama ilivyokusudiwa.
Pamoja na hayo, ameagiza Wakurugenzi kusimamia mikopo ya asilimia 10 na kuondoa changamoto zinazolalamikiwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyoandaliwa kusimamia mikopo hiyo.