Waandikishaji Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya Bayometriki kutoka Jimbo la Ukonga Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaa wakila kiapo cha kujitoa uanachama na kile cha kutunza siri leo Machi 14,2025 kabla ya kuanza kwa mafunzo ya siku mbili kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. (Picha na INEC).
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele (katikati) akizungumza na washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya Waandikishaji Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya Bayometriki kwa Jimbo la Ukonga Halmashauri ya Jiji la Daes Salaam alipotembelea mafunzo hayo Machi 14,2025. Kulia ni Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Dar es Salaam, Ndg. na Kushoto ni Afisa Mwandikishaji wa Jiji la Dar es Salaam, Adv. Faraja Nakua. (Pichja na INEC).
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya Waandikishaji Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya Bayometriki kwa Jimbo la Ukonga Halmashauri ya Jiji la Daes Salaam wakiwa katika mafunzo hayo. (Picha na INEC).
……
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka Waandikishaji Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya Bayometriki (BVR) kutekeleza majukumu yao vituoni kwa kufuata sheria, Kanuni na Taratibu za Tume pamoja na umakini katika utunzaji vifaa.
Hayo yamesemwa leo Machi 14, 2025 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele wakati alipotembelea na kuzungumza na washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya Waandikishaji Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya Bayometriki kwa Jimbo la Ukonga Halmashauri ya Jiji la Daes Salaam.
“Katika kufanya kazi ambayo kwayo mnafundishwa hivi leo, mkafanye kwa kufuata Sheria, Kanuni na taratibu, vyote hivyo mtafundishwa lakini pale ambapo utaona umekwama usisite kuwasiliana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili usikwamishe zoezi,” alisema Jaji wa Rufani Mwambegele.
Aidha, Jaji Mwambegele aliwataka washiriki ambao ndio wanakwenda kutekeleza jukumu la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha wanatunza vifaa watakavyo kabidhiwa.
Jaji Mwambegele alisema vifaa hivyo vimetumika nchi nzima kwa mizunguko 12 ambayo Tume iliipanga na sasa ipo mzunguko wa 13 unaotaraji kutekelezwa Mkoani Dar es Salaam kuanzia Machi 17 hadi 23, 2025 kwa kutumia vifaa hivyohivyo na vinapaswa kutunzwa kwani vitatumika pia katika awamu ya pili ya zoezi la uboreshaji nchi nzima.
“Vifaa hivi isingekuwa kutunza vyema msingekuwa hapa leo, vifaa hivi vimenunuliwa na kodi za wananchi kwa bei ya juu sana hivyo nawaomba mvitunze vifaa hivi kwanza wakati huu wa mafunzo lakini pili wakati wa zoezi lenyewe,” alisema Jaji Mwambegele.
Mapema akifungua mafunzo hayo baada ya kuwaapisha washiriki hao kiapo cha kujitoa unachama na kile cha kutunza siri, Afisa Mwandikishaji wa Jiji la Dar es Salaam, Adv. Faraja Nakua aliwataka washiriki hao kufanya kazi kwa weledi na kuwa na lugha nzuri kwa wananchi.
“Mtakapokua vituoni zingatieni weledi wa kazi, nidhamu, kujituma na bidi ya kazi na lugha nzuri kwa wateja wetu, wateja wetu ni Wapiga Kura watakao jitokeza kwaajili ya kuboresha au kujiandikisha au kutoa taarifa za kufutwa kwa mpiga Kura aliyepoteza sifa ya kuwepo kwenye Daftari,”alisema Nakua.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoanza leo Machi 14 na kutaraji kutamatika Machi 15 mwaka huu ni maandalizi kuelekea zoezi la Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura Mkoa wa Dar es salaam kuanzia Machi 17 hadi 23,2025.