Na. Peter Haule, Nyanduga Mara, WF
Baadhi ya Wazee wa Kijiji cha Nyasoko na Nyanduga Kata ya Koryo, Wilayani Rorya Mkoani Mara m, wameeleza shauku yao ya kuona elimu ya fedha inawafikia zaidi vijana ambao wanatafuta fedha kwa bidii lakini hawaendelei kiuchumi kutokana na kukosa elimu ya fedha.
Hayo yameelezwa na Wazee wa Vijiji hivyo akiwemo Mzee Cleophas Otieno Obelo, Ray Abich na Mchungaji Thomas Msoke, wakati Timu ya Wataalamu wa elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, ikiongozwa na Bw. Salim Khalfan Kimaro ilipofika katika kata hiyo, kutoa elimu ya fedha.
Walisema kuwa vijana hawana elimu ya fedha na wanapoteza mali nyingi wanazotafuta kwa jasho kwa kukosa maarifa na kushauri elimu inayotolewa sasa ifike vijiji vyote ili vijana waweze kujinasua kwenye changamoto ya maisha.
Wazee hao waliipongeza Serikali kwa kutoa elimu ya fedha kwa kuwa wamepata maarifa ambayo hawakuyatarajia, hivyo wangependa vijana wengi washiriki katika mafunzo hayo kwa kuwa wana nafasi ya kufanya mambo makubwa kwa maisha yao ya baadae.
Akizungumza kuhusu elimu aliyoipata, Mzee Cleophas Otieno Obelo, alisema kuwa licha ya umri wake kuwa mkubwa anakwenda kuweka mambo sawa na ana uhakika wa kuongeza kipato kwa kuwa yeye ni mjasiriamali wa muda mrefu kuanzia mwaka 1981 lakini mikopo isiyofaa na ukosefu wa elimu ya namna bora ya kuwekeza vilikuwa changamoto katika shughuli zake.
“Elimu imetupatia mwanga mkubwa, kwa muda uliobaki tunaweza kuwekeza kwa maisha ya uzeeni wakati huu ambao nguvu zinaelekea kuisha na kushindwa kushiriki katika kutafuta kipato ukilinganisha na vijana”, alisema Mzee Obelo.
Alisema kabla ya elimu hiyo wamekuwa wakishuhudia watu wengi wakidhurumiwa hususani wanaokopa katika taasisi zisizosajiliwa rasmi, hivyo elimu hiyo imetoa mwelekeo wa eneo zuri la kukopa ili kuepukana na mikopo isiyo na faida.
Aidha, aliwashauri wananchi wanaokopa katika maeneo yasiyo rasmi kuacha kukopa katika maeneo hayo kwa kuwa madhara yake ni makubwa.
Kw upande wa wakina mama wa eneo hilo akiwemo Bi. Judithi Zephania na Matha Joseph, walisema kuwa, wao ndio waathirika wakubwa wa mikopo umiza kutokana na kutozwa riba kubwa, jambo linalosababisha kushindwa kuirejesha na kuwa chanzo cha migogoro ya familia, ila kwa sasa wanaweza kuwatumia maafisa maendeleo kupata mwongozo wa namna bora ya kukopa kwa kuwa wamepata elimu.
Kwa upande wake Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, alisema kuwa miongoni mwa chanzo kikubwa cha mikopo yenye riba kubwa ni tabia ya watu kutojiwekea akiba, hivyo wanapopata uhitaji wa ghafla wanajikuta wanakopa bila kuwa na uelewa na kusababisha changamoto.
Alisema kuwa elimu itaendelea kutolewa kwa kuwa ni program endelevu, lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata elimu na kumudu vema shughuli zao za kujipatia kipato.
Zoezi la kutoa elimu ya fedha linaendelea kwa rika zote katia vijiji na Kata za Wilaya zilizopo Mkoani Mara ikiwa ni pamoja na Wilaya za Rorya, Musoma, Bunda, Butiama

Mzee Ray Abich na Cleophas Otieno Obelo (kulia), wakipata elimu ya fedha, Mkoani Mara, zoezi linalofanywa na Timu ya Wataalamul kutoka Wizara ya Fedha, Mkoani Mara.





Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyahela Shirati Kata ya Tai, Rorya, Mkoani Mara, Bw. Joseph Omuga Sausi, akiuliza swali kuhusu usajili wa huduma ndogo za fedha, wakati wa zoezi la kutao elimu ya Fedha katika Kata hiyo Mkoani Mara, linalofanywa naTimu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha.
(Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Rorya)