Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Joseph Holle Makungu akizungumza na waandishi wa habari Machi 14, 2025 jijini Dar es Salaam.
……..
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke inamchunguza Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Habibu Mchange kwa tuhuma za kuwaandaa baadhi ya viongozi wa CCM Kata ya Tungi Wilaya ya Kigamboni kwa ajili ya kuwapatie fedha ili wampige kura kitenda ambacho ni kinyume na sheria ya uchaguzi ya mwaka 2024 na kanuni ya chama cha CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 14, 2025 jijini Dar es Salaam Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Joseph Holle Makungu, amesema kuwa mnamo Machi 13 mwaka huu walipokea taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa kuna mwanachama wa CCM Habibu Mchange ambaye ni miongoni mwa watu wanaotarajia kutia nia ya ugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Kigamboni katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Makungu amesema kuwa Mchange sio mtekelezaji wa ilani ya chama kwa kuwa sio kiongozi, Diwani au Mbunge kupitia chama hicho, huku akieleza kuwa kwa sasa kanuni ya 69 (6) kuhusu uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola inaeleza : ni marufuku kwa mwanachama yoyote anayetarajia kugombea au wakala wake kutoa misaada wakati wa uchaguzi unapokaribia.
“TAKUKURU walifika ofisi ya CCM Kata ya Tungi na kubaini baadhi ya viongozi wa CCM walikubaliana kukutana na Habibu Mchange, baada muda gari aina ya luger yenye namba T366 EBL iliyombeba Mchange iliwasili kwenye maegesho ya magari ya ofisi hiyo ya CCM, baadhi ya viongozi wa CCM hawakutoa ushirikiano kwa Maafisa wa TAKUKURU hivyo waliondoka nao kwa ajili ya mahojiano na wote walisema kikao hicho hakikua halali” amesema Makungu.
Katika hatua nyengine Makungu amekanusha taarifa zilizotolewa katika gazeti la Jamvi la Habari toleo namba 2550 la 14/03/2025 kwamba TAKUKURU inatumiwa na wanasiasa wanataka kutia nia ya kugombea nafasi katika uchaguzi mkuu ujao kuwa sio kweli hivyo ni upotosha umma.
“Gazeti hilo pia limetoa taarifa ya upotoshaji kuwa TAKUKURU waliwafungia viongozi wa CCM wakiwa katika kikao cha kupanga uhamasishaji wa uandikishaji daftari la wapiga kura, TAKUKURU inafuatilia kwa karibu wote wanaodaiwa kufanya kampeni kabla ya muda kwa kutoa rushwa kwa wapiga kura Jimbo la Kigamboni na Tanzania kwa ujumla” amesema Makungu.