Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Ally Ngeruko ameitaka jamii kulipa kodi kwa hiari na uaminifu ili nchi iendelee kujengwa kwani ni lazima ijengwe kwa mapato yatokanayo na kodi.
Ngeruko ametoa wito huo Machi 14,2025 wakati wa hafla fupi ya Iftari iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dar es Salaam.
“Nchi haijengwi kwa udongo bali kwa mapato, hivyo watoto wakijengewa utamaduni wa kulipa kodi kama ilivyo kwa wazazi wao nchi itaendelea kujengwa na ulipaji kodi kwa hiari na kwa uaminifu utafuatwa na hili litafanikwa endapo mtawarithisha watoto wenu utamaduni huu,”amesema Ngeruko
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amewataka viongozi wa dini kuhamasisha waumini wao kulipa kodi ili kuleta maendeleo kwa taifa kwani suala la kulipa kodi ni wajibu uliohimizwa kwenye dini zote.
“Kulipa kodi ni halali kwa mujibu wa dini zetu basi tutekeleze hili bila kusukumwa,tumekaa hapa ukumbini kwa amani kwa sababu kuna ulinzi na usalama, hayo ni matokeo ya kodi, kila mmoja amefika kupita barabarani nazo zimejengwa kwa kodi, Elimu bure inayotolewa kwa watoto wetu nayo ni matunda ya kodi hivyo tuendelee kuchangia katika kulipa Kodi ” amsema Mwenda.
Mwenda amesema katika kipindi hiki cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na Kwaresima, matumizi ni makubwa hivyo wananchi wanaweza
kuisaidia nchi kwa kudai risiti kila wanapofanya manunuzi kwa kufanya hivyo ni ibada na utapata thawabu pamoja na kuchangia nchi.
Aidha, Mwenda amewahimiza Watumishi wa TRA kuendelea kutenda haki na kuwa waadilifu wanapokuwa kwenye shughuli za ukusanyaji kodi na kuchukua kilichopo haki kwa Mamlaka na si vinginevyo .
Amesema kuwa mwenendo wa Mamlaka hiyo unaridhisha kwa kuwa watumishi wa Mamalaka hiyo hawajakenguka na kuacha misingi ya uadilifu.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Omar, ametoa wito kwa Waislam wote ndani ya mkoa wa Dar es Salaam kulipa kwa kuwa dini inahimiza ulipaji kodi .
“Najua umuhimu na lengo la TRA ni kukusanya mapato ya nchi yetu kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu kama Sheikh wa mkoa nahimiza waislam wote, taasisi na misikiti tujitokeze katika kuwasaidi TRA katika kukusanya mapato hakuna chochote kitachofanyika …tutakuwa tunahimiza kama ambavyo tunahimizwa kutoa zaka halali,”amesema Omar.