Na WAF – Dar es Salaam
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amewaasa waumini wa dini zote nchini na jamii kwa ujumla kuendelea kuomba na kuchukua tahadhali dhidi ya ugonjwa wa Mpox bila na kujengeana hofu na kuogopeshana kwani ugonjwa huo ukiwahi mapema unatibika.
Dkt. Magembe ameyasema hayo Machi 15, 2025 wakati wa ibada ya Sabato katika kanisa Magomeni Jijini Dar es Salam na kubainisha tahadhali ambazo jamii zinatakiwa kuchukua wakati ikiendelea na maombi na kapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Dkt. Magembe amesema kwa sasa jamii inatakiwa kuchukua tahadhari kwa kubadili mtindo wa maisha katika kipindi hiki ili kuepuka tabia ambazo zitachochea kusambaa kwa ugonjwa huo.
Dkt. Magembe amebainisha tahadhari hizo ni pamoja na kuwahi katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu unapoona mojawapo ya dalili za ugonjwa wa Mpox au kupiga simu nambari 199 bila malipo sambamba na kuepuka kugusana kwa kupeana mikono, kuepuka kugusa majimaji ya mwili ya mtu mwenye dalili za Mpox na kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.
Awali Dkt. Magembe amebainisha dalili za ugonjwa wa Mpox ni pamoja na homa, maumivu ya kichwa, uvimbe, maumivu ya mgongo na misuli kuuma mara baada ya homa , upele unaweza kutokea na kuonekana kama lengelenge au tetekuwanga.
Pia Dkt. Magembe amezigusa jamii za wawindaji kuchukua tahadhali katika mawindo yao kwa kuepuka kushika mizoga ya aina yoyote kwani kufanya hivyo kutaharisha usalama wa afya zao na jamii inayowazunguka.
Mpox ni ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Monkeypox ambao ulitangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama dharura ya Afya ya Kimataifa (PHEIC) mnamo Agosti 2024, Tarehe 10 Machi 2025, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitangaza kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa huo wa Mpox, Serikali ya Tanzania inaendelea kutekeleza afua za afya ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia Kanuni za Afya za Kimataifa za mwaka 2005.