Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa, Maendeleo, na Diaspora, Mhe. Neale Richmond, amefanya ziara ya siku moja mkoani Tanga ambako amekutana na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Dkt. Batilda Buriani.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wameangazia namna ya kuendelea kushirikiana kupitia sekta za kimkakati, ikiwemo afya, ufugaji, uchumi wa bluu, uhifadhi wa mazingira ya pwani na baharini, uwezeshaji wa kijinsia, na maendeleo ya vijana.
Mhe. Dkt. Buriani ameishukuru Serikali ya Ireland kwa mchango wake katika miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo , hasa katika sekta za afya, ufugaji, na uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake na vijana.
Ameeleza dhamira ya mkoa wa Tanga kuendele kushirikiana na Ireland ili kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa Ireland kuangazia fursa za uwekezaji katika sekta za utafiti wa maziwa, uvuvi, na afya, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uchumi wa bluu kama nyenzo ya maendeleo endelevu katika mkoa huo.
Kwa upande wake, Mhe. Richmond ameahidi kuendeleza ushirikiano kati ya Ireland na Tanzania, akisisitiza kuwa nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika sekta za afya, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na mifugo.
Katika ziara yake mkoani Tanga, Waziri Richmond ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, ambaye pia anawakilisha Ireland, Mhe. Mbelwa Kairuki, Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Nicola Brennan, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme, pamoja na maafisa wengine wa serikali kutoka Tanzania na Ireland.