Hawa Halifani Mbega mkazi wa Mtaa wa Mnazi Mmoja Kata ya Jangwani Dar es Salaam akifurahia kadi yake mpya ya Mpiga Kura baada ya kukabidhiwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa Jacobs Mwambegele. Mkoa wa Dar es Salaam umeanza leo uboreshaji wa Daftari na utadumu kwa siku saba hadi Machi 23 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa Jacobs Mwambegele leo Machi 17, 2025 ametembelea baadhi ya vituo vya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani Dar es Salaam na kushuhudia mwenendo wa zoezi hilo katiuka siku ya kwanza. Mkoa wa Dar es Salaam umeanza leo uboreshaji wa Daftari na utadumu kwa siku saba hadi Machi 23 mwaka huu.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo wananchi wengi walionekana
kwa wingi vituoni kujiandikisha au kuboresha taarifa zao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi
17, 2025 baada ya kutembelea vituo vya Uboreshaji, Mwenyekiti wa Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele alisema zoezi
hilo limeanza vyema pasi na changamoto yeyote na kuwataka wananchi kuendelea
kujitokeza.
“Tume inaendelea na uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura na sasa tupo mzunguko wa 13 mkoani Dar es Salaam, nimeshuhudia
kuanza kwa zoezi katika kituo cha Mnazi Mmoja…watu wengi wamejitokezakuja kujiandikisha
na kuboresha taarifa zao,”alisema Mhe. Jaji wa Rufani Mwambegele.
Jaji wa Rufani Mwambegele amesema mwitikio wa
wananchi ni mkubwa na ameshauri wananchi wa Dar es Salaam kuzitumia siku za
mwanzo za uboreshaji ili kuepusha msongamano kwa siku za mwishoni mwa zoezi.
“Nawasihi watanzania wale wanaostahili
wajitokeze kwa wingi kuja kuboresha taarifa zao au kujiandikisha, leo tarehe 17
mwezi huu wa tatu, 2025 ndio siku ya kwanza mwisho tarehe 23 mwezi huu wa tatu
2025 sasa tunakawaida ya kusubiri siku za mwisho hivyo nawasihi waje siku hizi
za mwanzo,” alisema Jaji Rufaa Mwambegele.
Nae Afisa Mwandikishaji wa Halmashauri ya
Manispaa ya Kinondoni yenye Majimbo ya Kawe na Kinondoni Ndg. Omary Mkangama
amesema zoezi hilo limeanza vizuri na hali ni shwari na wananchi wanapata
huduma vizuri.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inataraji
kuandikisha Wapiga Kura wapya 643,420 mkoani Dar es Salaam ambapo jumla ya
vituo 1,757 vinatumika kwenye
uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 96
katika vituo 1,661 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka
2019/20.
Aidha Tume imejipanga kikamilifu kuhakikisha
wananchi wote wenye sifa za kuandikishwa wanaandikishwa kwani BVR zaidi ya
5,000 na watendaji wa kutosha wapo kwaajili ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Tume imeshakamilisha uboreshaji wa Daftari
katika Mikoa 29. Kwa mujibu wa ratiba, leo Tume inaanza uboreshaji katika mzunguko
wa 13 ambao ni mzunguko wa mwisho wa uboreshaji wa Daftari. Mzunguko huu
unahusisha Mkoa wa Dar es Salaam pekee.
Kailima amesema kwa mkoa wa Dar es Salaam
Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 643,420 ikiwa ni sawa na ongezeko
la asilimia 18.7 ya wapiga kura 3,427,917 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura.
Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa
Dar es Salaam utakuwa na wapiga kura
4,071,337 idadi ambayo inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo
watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa
uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine
hawakuweza kujiandikisha.
Zoezi la uboreshaji wa Daftari linahusu
kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18
na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka
2025, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika
na kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo
majina na taarifa nyingine.
Uboreshaji wa Daftari pia unahusu kutoa fursa
kwa wapiga kura waliopo kwenye Daftari na ambao wamehama, waweze kuhamisha
taarifa zao kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa wapiga kura
waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa
ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania na kifo.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Balozi Omar Ramadhan Mapuri leo tarehe 17 Machi, 2025 ametembela vituo mbalimbali vya kuandikisha Wapiga kura vya Jimbo la Kibamba Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Mkoa wa Dar es Salaam kuona zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linavyoendelea.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Balozi Omar Ramadhan Mapuri leo tarehe 17 Machi, 2025 ametembela vituo mbalimbali vya kuandikisha Wapiga kura vya Jimbo la Kibamba Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Mkoa wa Dar es Salaam kuona zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linavyoendelea.
Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika vituo vya Kuandikishia na kuboresha taarifa za Wapiga Kura.