MKURUGENZI wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 17,2025 jijini Dodoma kuhusu mafanikio na mwelekeo ya Mfuko huo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
MKURUGENZI wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 17,2025 jijini Dodoma kuhusu mafanikio na mwelekeo ya Mfuko huo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha amesema kuwa wanaisubiri Serikali kujibu ombi lao la kubadilisha sheria za malipo ya fao la kupoteza ajira kwa waajiriwa wenye elimu ya kuanzia Diploma ili waweze kuwalipa mafao yao yote kwa mara moja.
Amesema kuwa utaratibu uliopo sasa kwa mwajiriwa anayepoteza ajira anayestahili kulipwa mafao yote ni yule mwajiriwa ambaye elimu yake haijafika Diploma.
Amesema kwamba NSSF imejiridhisha kuwa inaweza kulipa fedha yote ndani ya miezi mitatu toka mwajiriwa apoteze ajira pale atakapoomba kupata mafao yake.
“Tumeomba mabadiliko ya sheria tulivyoona tunaweza kulipa fedha yote kwa wale waajiriwa wenye elimu ya Diploma wanaopoteza ajira zao.Serikali ikikubali tutalipa yote ndani ya miezi mitatu toka mwajiriwa apoteze ajira,”amesema Mshomba.
Vilevile Mshomba amesema kuwa maboresho yaliyofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita yamekuwa na mchango chanya na wenye manufaa katika ukuaji wa Mfuko ambapo amesema mwenendo mzuri wa ukuaji umechangiwa na ongezeko la asilimia 92 katika thamani ya Mfuko Katika kipindi husika.
Amesema kuwa thamani ya Mfuko imeongezeka kwa asilimia 92 kutoka TZS bilioni 4,836.73 mwezi Februari 2021 hadi kufikia TZS bilioni 9,299.39 mwezi Februari 2025.
“Ongezeko hili limechangiwa na kuongezeka kwa wanachama, mapato yatokanayo na michango na kukua kwa thamani ya vitegauchumi vya Mfuko. Mwenendo mzuri wa ukuaji wa Mfuko unaashiria uhimilivu na uendelevu imara wa Mfuko ya wanachama,”amesema Mshomba.
Aidha Mshomba amesema kuwa malipo ya mkupuo wa awali wa Mafao umeongezeka na kiwango cha kima cha chini cha pensheni ya kila mwezi kimeboreshwa Katika kipindi husika, Mfuko ulilipa mafao ya bilioni 3,108.89 na malipo ya mafao kwa mwaka yaliongezeka kwa asilimia 69 kutoka bilioni 537.08 katika mwaka ulioishia Februari 2021 hadi kufikia bilioni 909.16 katika mwaka ulioishia Februari 2025.
“Kutokana na utendaji uliotukuka wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwajali wastaafu, Mfuko umeendelea kuboresha tena ulipaji wa mafao kwa wanachama wote waliokuwa wanalipwa mkupuo wa awali wa asilimia 33 na kwanzia mwezi Julai 2022, waliongezewa kiwango cha mkupuo kufikia asilimia 35. Uamuzi huu wa Serikali wa kuongeza kiwango cha malipo ya mkupuo kwa wanachama wa NSSF pia umezingatia uendelevu wa Mfuko wetu,”amesema Mshomba.
Pamoja na hayo Mshomba amezungumzia matarajio ya Mfuko huo ambapo amesema kwa mujibu wa mpango wa mwaka wa fedha 2024/25 ni
kuendelea kutekeleza mikakati ya ukuaji wa Mfuko ili ufikie thamani ya trilioni 11,000.00 mwezi Juni 2026,ikiwa ni mara mbili ya thamani ya trilioni 5,068.82 iliyofikiwa mwezi Juni 2021.
Pia amesema kuendelea kubaini fursa za uwekezaji katika maeneo mapya yenye faida zaidi na salama ikijumuisha masoko ya hisa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC ili kuweka mtawanyo mzuri wa vitega uchumi.
“Tarajio lingine ni kuimarisha mifumo na matumizi ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi, kupunguza malalamiko kwa wateja, kutoa huduma bora kwa wanachama wake na kuendelea kutekeleza Mpango wa uchangaiji wa hiari wa Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi waliojiajiri,”amesema Mshomba.