Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kuilinda misingi inayoiongoza sekta ya ardhi ili kuhakikisha kuwa Watanzania wananufaika na rasilimali hiyo, na amesisitiza kuwa ardhi yote ni mali ya umma wa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Sharifa B. Nyanya imesema Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995, Toleo la Mwaka 2023 iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa, maboresho ya Sera hiyo yataimarisha utendaji kazi katika sekta ya ardhi kwa kuimarisha matumizi ya TEHAMA na mifumo pamoja na kuimarisha uwezo wake wa utatuzi wa migogoro, hatua itakayohusisha pia kupitia upya mfumo wa Mabaraza ya Ardhi na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa vyanzo vya migogoro ya ardhi.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewataka watumishi kwenye sekta ya ardhi kubadilika na kufanya kazi kwa weledi na kwa haki na amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi kuchukua hatua stahiki kuwawajibisha watumishi wote wanaokwamisha utendaji wa Wizara hiyo.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amesema kuwa maboresho hayo yamewezesha kujumuisha masuala muhimu ambayo hayakuwemo kwenye toleo la 1995 ikiwemo uimarishaji wa mipaka ya kimataifa, upimaji wa ardhi katika maji ili kukuza uchumi wa buluu na usimamizi wa biashara ya sekta ya milki.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema kuwa Sera ya Ardhi iliyoboreshwa imeweka sharti la kuwataka wamiliki kusajili ardhi zao na ili kuimarisha usalama wa milki, Serikali inataka kila kipande cha ardhi nchini kipangwe, kipimwe na kisajiliwe.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa ili kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya milki hususan makazi ya bei nafuu, Sera iliyoboreshwa inaweka utaratibu wa kuwezesha waendelezaji milki wa kigeni kuwekeza katika sekta ya nyumba na kuuza kwa wenye uhitaji.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amesema kupitia Sera hiyo Serikali inaenda kuchochea ushirikishwaji zaidi wa sekta binafsi katika sekta ya milki, hususan ujenzi wa makazi ya bei nafuu maeneo ya mijini na vijijini, hatua inayolenga pia kuimarisha uwezo wa wananchi wote na hasa vijana wanaoanza maisha kupata makazi kwa bei nafuu.