*Airtel, UNICEF zawezesha Mtandao wa Kasi kwenye Shule 50 wilayani Ukonga, jijini Dar es Salaam
*Airtel, UNICEF kutoa intaneti ya BURE kupitia mradi wa Airtel SmartWASOMi
Dar es Salaam, Machi 2025.
Airtel Tanzania imewezesha mtandao wa intaneti wa kasi ya juu kwa shule za sekondari 50 wilayani Ukonga, Dar es Salaam kupitia mpango wa Airtel SmartWasomi wa kuunganisha shule 3,000 na elimu ya kidijitali ndani ya miaka tano.
Hatua hiyo pia inaenda sambamba na malengo Mheshimiwa Waziri wa TEHAMA, Jerry Silaa ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga baada ya kuahidi kuboresha mazingira ya kufundisha na kujisomea kwa kuleta mifumo ya kidijitali kama njia ya kukabiliana na uhaba wa vifaa vya kufundishia.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo vya intaneti iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Pugu wilayani Ukonga, Meneja Uhusiano wa Umma kutoka Airtel Tanzania, Jackson Mmbando, alisema kuwa, “Airtel SmartWASOMI ni mpango ambao umelenga kuboresha sekta ya elimu kwa kuongeza kasi ya kujifunza kidijitali kote nchini Tanzania. Mradi huu unatekelezwa kwa kushirikiana na serikali kupitia Wizara ya Elimu na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF). Airtel SmartWASOMI imelenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa walimu na wanafunzi. Tunaunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha elimu ya kidijitali kwa wanafunzi kote nchini.”
“Sambamba na washirika wetu, tuko mbioni kufunga router za Airtel Tanzania zenye mtandao wa kasi kwenye shule zaidi ya 3,000 ili kuwarahisishia walimu na wanafunzi kupata vifaa muhimu vya kujifunzia bila gharama yoyote. Kupitia maktaba ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) wanafunzi na walimu wataweza kupata vitabu na nyenzo mbalimbali za kujisomea na kujifunzia kwa urahisi kupitia intaneti ya kasi ya Airtel,” alieleza Mmbando.
Mmbando aliongeza kuwa, “Airtel imesambaza na kufunga vifaa vya intaneti ya Airtel katika shule 50 za sekondari zinazomilikiwa na Serikali Wilayani ya Ukonga kupitia mradi wa huo.”
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Elimu ya Sekondari Mwalimu Mussa Ali aliwataka walimu aliwasisitiza walimu kutumia fursa hiyo vizuri kwasababu uwepo wa mawasiliano ya intaneti utawawezesha kuweka taarifa nan akala mbalimbali zitazowasaidia wanafunzi kujisomea.
“Kuunganishwa kwa router hizi kwenye shule zetu kunawapa walimu fursa ya kutumia kama nyenzo ya kufundishia wanafunzi mtandaoni. Mpango huu ni muhimu katika kukabiliana na uhaba wa vifaa vya kufundishia lakini pia rasilimali nyinginezo katika shule zetu, kwa masomo ya fizikia, Kemia, baiolojia na hisabati. Kupitia intaneti hii, walimu wataweza kuwafundisha wanafunzi wao hata wakiwa mbali,i” alisema Ali.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Buyuni, Asha Kinyogo, aliipongeza Airtel Tanzania kwa kuwekeza katika kizazi cha sasa na kijacho kwa kuwezesha upatikanaji wa nyenzo za elimu kwa urahisi kupitia teknolojia ya mtandao.
“Naipongeza Airtel kwa kuja na mpango huu wa kubadilisha maisha unaoleta sura mpya ya sekta ya elimu nchini Tanzania. Ufungaji wa intaneti ya Airtel katika shule yetu utaboresha uzoefu wa elimu kwa wanafunzi, kwani nyenzo zote za elimu sasa zinapatikana kwao kupitia maktaba ya mtandaoni. Tunaamini mradi wa Airtel SmartWasomi utaleta matokeoi kubwa kwa shule zetu,” alibainisha.
Utekelezaji wa mpango wa miaka mitano wa SMARTWASOMI unadhihirisha dhamira ya Airtel Tanzania kusaidia wanafunzi wa Kitanzania kufikia uwezo wao kamili kwa kutoa fursa sawa ya kujifunza kwa njia ya kidijitali.
Kampuni ya Airtel Tanzania kupitia Smart WASOMI tayari imefunga Mtandao wa Bure kwa ajili ya kujifunzia kupitia maktaba ya TIE na Shule Direct kwa shule 50 za visiwani Zanzibar, 42 mkoani Kilimanjaro, 50 Arusha, 15 Nzega-Tabora, 15 Dodoma na 20 katika shule za Mbeya. Mradi huu bado unaendelea ili kuhakikisha shule 3,000 za sekondari za Serikali zinazunganishwa na intaneti kwa ajili ya kujifunza kidijitali.