Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu amesisitiza Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi katika utumishi wa umma kusimamia rasilimaliwatu vyema ili iweze kusimamia rasilimali nyingine za taifa kikamilifu.
Mhe. Sangu amesema hayo leo Machi 18,2025 Jijini Mwanza wakati akifungua kikao kazi chenye lengo la kutambua changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298.
“Iwapo rasilimaliwatu itasimamiwa vibaya matokeo ya utendaji kazi yatashuka na uchumi hauwezi kukua, hivyo taifa litashindwa kufikia malengo yake ya kutoa huduma bora kwa umma” alisema Mhe. Sangu.
Aidha, amewataka baadhi ya washiriki hao kujitathimini na kuacha tabia ya kukiuka Sheria, Kanuni, Taratibu na Miiko ya kazi katika Utumishi wa Umma kwa kuwa inasababisha malalamiko, usumbufu na migogoro isiyokuwa ya lazima mahala pa kazi.
“Ninyi maofisa mumepewa dhamana ya kutekeleza majukumu ya kusimamia rasilimaliwatu ili kupata matunda chanya, hivyo mnapaswa kushirikiana na kuwa wabunifu ili kukabiliana na changamoto zilizopo” alisisitiza Mhe. Sangu.
Naye, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Cyprus Kapinga amesema kuwa Ofisi yake inapokea barua zikiomba ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi ambayo yameshatolewa maelekezo. Huo ni ushahidi kuwa maofisa hao hawawajibiki ipasavyo katika kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu mbalimbali za kiutumishi.
Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bibi. Hilda Kabissa alisema kuwa mada mbalimbali zitawasilishwa na kufuatiwa na majadiliano kwa lengo la kuwajengea washiriki uelewa wa Taratibu mbalimbali zinazopaswa kuzingatiwa katika utendaji kazi.