Katikati ni mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile wakati akizungumza na wadau wa afya juu ya namna ya kujikinga na Mpox
Wadau mbalimbali wa afya walioshiriki katika kikao hicho
Baadhi ya viongozi wa dini walioshiriki katika kikao hicho
……………
Na Neema Mtuka Sumbawanga,
Rukwa: Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Ally Chirukile, amekutana na wadau wa afya na maendeleo kwa mazungumzo kuhusu elimu ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya nyani Monkeypox (M-POX).
Nyakia amewahimiza wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa mpox kwa kuepuka kushiriki vitu binafsi kama nguo ,mashuka, msawaki vilivyotumiwa na mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Katika kikao hicho, wadau wamejadili mbinu bora za kuelimisha jamii kuhusu dalili, njia za maambukizi, na hatua za kujikinga na ugonjwa huo.
Chirukile amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na jamii ili kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi kwa wakati Pia, ametoa wito kwa mamlaka za afya kuimarisha ufuatiliaji na uhamasishaji wa jamii kuhusu njia bora za kujikinga na kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.
Wadau wa afya walitoa mapendekezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vyombo vya habari kueneza elimu, kampeni za uhamasishaji mashuleni na katika jamii, pamoja na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa visa vya ugonjwa huo.
Meshaki Ibrahimu ni mdau wa afya anasema kuna umuhimu wa kufuata kanuni za kujikinga kwa kuwa mpox ni ugonjwa unaoharibu mwonekano wa mtu kwa kutoka vipele vinavyotoka kwenye mwili wa mtu hivyo kuweza kusababisha maambukizi.
“Ni muhimu elimu ikatolewa kwa wananchi hasa kwenye mikusanyiko ya watu bila kuwasahau watoto shuleni ili wajue namna ya kujikinga na kuacha tabia ya kupeana vitu ovyo jambo ambalo litawafanya wabaki salama”.amefafanua Ibrahim.
Kikao hiki ni sehemu ya juhudi za Wilaya ya Sumbawanga kuhakikisha afya za wakazi wake zinalindwa dhidi ya magonjwa yanayoibuka, huku ikisisitiza mshikamano wa pamoja katika kukabiliana na changamoto za kiafya.
Awali akizungumza katika kikao hicho mchungaji wa kanisa la kiinjili la kilutheri KKKT usharika wa lutha na mkuu wa jimbo la Sumbawanga Nicolaus Mero amesema ataitumia nyumba ya ibada kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wauumini ili waweze kujikinga na ugonjwa huo.
“Serikali iongeze jitihada za ufuatiliaji wa ugonjwa huo pia kuendelea kuimarisha uchunguzi mipakani hasa ukizingatia mkoa wa Rukwa unapakana na nchi jirani za kongo na Rwanda kwa kuwafanyia vipimo wageni wanaoingia nchini”.amesema Mero
Aidha mganga Mkuu wa Manispaa Sumbawanga, Daktari, Robert Rwebangira, amesisitiza kuwa serikali na wadau wa afya, wameendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha hatua za kujikinga zinachukuliwa kikamilifu.
Mkoa wa Rukwa unapakana na nchi mbili jirani, Zambia upande wa kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) upande wa magharibi kupitia Ziwa Tanganyika.
Kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu na shughuli za kibiashara kati ya Tanzania na nchi hizi jirani, kuna haja ya kuchukua tahadhari zaidi katika kudhibiti maambukizi ya magonjwa ya mlipuko kama M-POX.