Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WANAFUNZI wa shule ya sekondari Ewong’on iliyopo Kijiji cha Kambi ya Chokaa Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imepongezwa kutokana na ufaulu bora wa kidato cha nne kwa mwaka 2024.
Diwani wa Kata ya Naisinyai Mhe Taiko Kurian Laizer ametoa pongezi hizo kwenye sherehe za kuwakaribisha rasmi wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2025.
Taiko amesema wanafunzi wa kidato cha nne wa shule hiyo kwa mwaka 2024 wamefanya ufaulu bora kuliko shule zote za Wilaya ya Simanjiro.
“Matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2024 ufaulu bora umetokea shule ya Ewong’on wakiwa na daraja la kwanza yenye alama 10,” amesema Mhe Taiko.
Amesema kwenye wilaya ya Simanjiro hakuna shule yenye mwanafunzi aliyepapata ufaulu wa daraja la kwanza yenye alama 10.
“Ufaulu huo umetokana na juhudi kubwa ya walimu na uongozi wa shule wakiongozwa na mkuu wa shule William Ombay na wanafunzi kwa ujumla,” amesema Taiko.
Katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Mosses Makeseni amesema hatua hiyo ya ufaulu bora wa shule hiyo inaonyesha kuwa inapiga hatua katika upande wa taaluma.
“Tunawapongeza walimu, wanafunzi, wazazi na walezi kwa kuwaleta wanafunzi kwenye shule hiyo iliyowatoa kimasomaso na kuipa sifa kata ya Naisinyai kupitia taaluma,” amesema Makeseni.
Mkuu wa shule ya sekondari Ewong’on mwalimu William Ombay amesema jumla ya wanafunzi 73 walifanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne kwa mwaka 2024.
Mwalimu Ombay amesema wanafunzi hao wameongoza kwa alama A katika masomo ya hesabu na fizikia na wanafunzi wote wamefaulu kwa asilimia 98.
Amesema kwenye mtihani huo wanafunzi wawili walipata ufaulu wa daraja la kwanza, wanafunzi saba ufaulu wa daraja la pili, wanafunzi 13 daraja la tatu na wanafunzi 51 daraja la nne.
Amesema siri ya mafanikio ya ushindi wao ni wanafunzi kufundishwa vyema, mtihani ya mazoezi ya kutosha na kufundishwa muda wa ziada.
“Walimu na wanafunzi walipewa zawadi kwa kufanikisha ufaulu huo na wanafunzi wengine wanaoendelea na masomo nao walipewa zawadi kama motisha kwao,” amesema.


