Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Tanga: Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Japhari Kubecha, Ameyasema hayo leo mchana wakati wa mahojiano na mwandishi wetu kuhusu uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema kuwa miaka minne ya uongozi wake imejawa na matumaini, faraja, maridhiano, na imekuwa ni kipindi cha mabadiliko makubwa kwa taifa la Tanzania.
“Miaka minne ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni miaka ya matumaini, miaka ya kufarijiana, na ni miaka ya kujenga upya taifa letu. Ni kipindi cha mabadiliko ambacho kimeleta nguvu mpya na matumaini kwa wananchi wa Tanzania,” alisema Kubecha.
Akiendelea, Kubecha alieleza kuwa Rais Samia amedhihirisha ushupavu wa kiuongozi, ueledi wa maarifa, ubunifu wa kiutendaji, na umakini wa kazi. Katika kipindi hiki, ameweza kutafsiri maono ya watangulizi wake kwa vitendo, kwa kuzingatia masuala ya kidiplomasia, kidemokrasia, kiuchumi, kisiasa, na kijamii.
“Rais Samia amekuwa mfano wa uongozi bora, na ameleta mifano ya ufanisi katika nyanja zote za taifa letu. Ameweza kutekeleza maono kwa ufanisi mkubwa, akionyesha kuwa ana uwezo wa kukabiliana na changamoto za uongozi,” alisema Kubecha.
Kubecha alifafanua zaidi akisema kuwa sote tumeshuhudia miradi mingi ya kimkakati ikikamilika ndani ya muda mfupi, huku mingine ikianza na kutekelezwa kwa mafanikio makubwa. Aliongeza kuwa miradi hii imekuwa na tija kubwa, ikiwa ni chachu ya maendeleo ya haraka kwa taifa.
“Miradi hii imekuwa na tija kubwa, ikiwa ni chachu ya maendeleo ya haraka. Waliokimbia nchi wameweza kurudi kwa kishindo, huku wakirejea kufanya shughuli zao za kisiasa na kimaendeleo. Hata hivyo, watu wengi ambao walikuwa hawajulikani sasa wamepata nafasi ya kujulikana. Hadhi na heshima ya nchi yetu imelindwa ipasavyo, na uhuru na usawa vimejengeka kwa undani zaidi,” aliongeza.
Akiendelea na maoni yake, Kubecha alisema kuwa yote haya ni kiashiria cha uwezo, umadhubuti, uimara na ufanisi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uongozi wake.
“Yote haya ni dalili za uongozi bora, umadhubuti, na ufanisi wa Rais Samia. Ni wazi kuwa ameweza kupokea na kutekeleza changamoto za uongozi kwa ufanisi na mafanikio makubwa,” alisema Kubecha.
Katika hatua nyingine, Kubecha alisisitiza kuwa Watanzania wanakila sababu za kumuamini Rais Samia kwa mara nyingine na kumpa duru ya pili ya uongozi wa taifa letu.
“Tunakila sababu za kumuamini kwa mara nyingine na kumpa duru ya pili ya uongozi wa taifa letu. Hakuna anayefananishwa wala anayekaribia kufikia kiwango cha uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika nafasi hii kwa sasa,” alisisitiza.