Mjumbe wa kamati ya utendaji Taifa ya Chama cha Walimu Tanzania anayewakilisha Mkoa wa Ruvuma Sabina Lipukila,akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Halmashauri ya Wilaya Songea.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Kapenjama Ndilea,kifungua Mkutano wa Chama cha Walimu wa Halmashauri ya Wilaya Songea katika Ukumbi wa Anglikana Songea mjini.
Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania Mkoa wa Ruvuma,wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile wa pili kushoto baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Chama hicho katika Ukumbi wa Anglikana Songea Mjini.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Kapenjama Ndile katikati,akiwa katika Picha ya pamoja na Viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania wa Mkoa wa Ruvuma na Wilaya ya Songea baada ya kufungua rasmi Mkutano Mkuu wa Chama hicho jana.
…………
Na Muhidin Amri, Songea
MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Kapenjama Ndile,ametoa Ushauri kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini, kutafakari upya kuhusu kuwepo kwa Chama zaidi ya kimoja cha wafanyakazi wa kada moja ili kuondoa migogoro na migongano inayochangia kushuka kwa nidhamu sehemu ya kazi.
Ndile amesema hayo jana,wakati akizungumza na walimu kwenye Mkutano wa mwaka wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Halmashauri ya Wilaya Songea uliofanyika katika ukumbi wa Kanisa la Anglikana mjini Songea.
Alisema,uwepo wa chama zaidi ya kimoja kinachohudumia walimu wale wale ambao ni watumishi wa Serikali inapelekea kuwa na mashindano kati ya kiongozi wa Chama kimoja na kingine hivyo kutoheshimiana na kushusha morali ya kazi kwa walimu.
“Kwa mfano unakwenda shule ya Sekondari Maposeni au Mfaranyaki unakutana na viongozi wawili wa chama cha wafanyakazi,mmoja anatoka Chama cha Walimu Tanzania na mwingine wa Chama iko kingine,hii inaleta madhara makubwa katika utendaji kazi kwenye sekta ya elimu”alisema Ndile.
Alisema,viongozi hao hawafanyi kazi ya kutetea maslahi ya walimu bali watafanyakazi kwa kushindani ili kupata wafuasi wengi zaidi,jambo ambalo ni kinyume na falsafa ya Chama cha wafanyakazi.
Alisema,msingi wa kuundwa kwa Chama cha Wafanyakazi ni kuunganisha nguvu zao ili wawe na sauti moja, lakini walimu kwa kupitia Chama chao wanakwenda kinyume hali iliyosababisha hata nidhamu kushuka kutokana na kugawanyika makundi mawili.
“Heshima ya walimu kwa sasa imeshuka kutokana na kuwepo kwa chama zaidi ya kimoja kinachotetea walimu hatua inayopelekea baadhi ya walimu kutoheshimiana sehemu ya kazi.”alisema Dc Ndile.
Amewataka Walimu kuungana na kuwa kitu kimoja na kutetea maslahi yao,kudumisha nidhamu na kuheshimu mamlaka za utezi ili kujenga kizazi chenye maadili mema na viongozi bora.
“Lazima mamlaka tuziheshimu, tuache tabia ya kutunishiana misuli,watu wa namna hii hasa Viongozi wanawaharibia nyinyi walimu, Serikali inawapenda sana ndiyo maana inaendelea kuboresha maslahi yenu ikiwemo suala la mishahara,mazingira bora ya kufundishia na kutoa vifaa vya kufundishia”alisema Ndile.
Awali Katibu wa Chama cha walimu Halmashauri ya Wilaya Songea Adriano Ngairo alisema, walimu zaidi ya 255 wamefukuzwa uanachama baada ya kwenda kinyume na maadili ya chama hicho.
Aidha alisema,katika kipindi cha miaka minne jumla ya walimu 440 wamepanda madaraja ya mseleleko,kuruhusu walimu kupandishwa madaraja kwa wakati kutokana na mwongozo na ameishukuru Serikali kwa maboresho hayo yaliyowezesha kurudisha moroli ya kazi kwa walimu.
Ngairo,ameipongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu hususani ukarabati wa madarasa,nyumb za walimu na ujenzi wa shule mpya zaidi ya 600 hapa nchini na kutoa fedha za uendeshaji wa taasisi(Captation) kwa shule zote nchini.
Ameiomba Serikali kupitia taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(TAKUKURU)na idara nyingine za Serikali kushiriki kwa pamoja kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa ujenzi wa miundombinu ya shule ili kuepuka migongano inayopelekea baadhi ya walimu kukamatwa kwa kuonekana kushindwa kusimamia miradi hiyo.