Msimamizi wa Uchaguzi wa Chama cha Walimu(CWT) Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma kitengo cha Wanawake Deograsias Haule,akitangaza matokeo ya Uchaguzi huo ambapo Mwalimu Ibula Nyoni amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kitengo hicho katika uchaguzi uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari Samia Suluhu Hassan.
Mjumbe wa kamati ya Utendaji Taifa ya Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Sabina Lipukila kushotoa,kikabidhi cheti kwa Mwalimu Amodzize Kinyamagoha baada ya kuibuka mshindi wa nafasi ya Ujumbe kwenye uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma kitengo cha Wanawake.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Ibula Ngonyani kulia,akipokea cheti maalum baada ya kuibuka mshindi wa nafasi hiyo kwenye Uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania kitengo cha Wanawake uliofanyika jana katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Samia Suluhu Hassan.
Na Mwandishi Wetu,
Namtumbo
MKUU wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Ngolo Malenya,amewapongeza walimu katika Wilaya hiyo kwa kutekeleza na kusimamia vizuri ujenzi wa miundombinu ya shule za Msingi na Sekondari.
Malenya,ametoa pongezi hizo jana wakati akifungua mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT) Wilaya ya Namtumbo uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Dkt Samia Suluh Hassan.
Alisema,walimu ni watu muhimu na msaada mkubwa kwa Serikali siyo katika kuwajengea uwezo watoto bali hata katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayopelekwa kwenye shule zao.
Hata hivyo alisema kuwa,Serikali haitosita kuwachukulia hatua walimu watakaoshindwa kusimamia ujenzi wa miundombinu ya shule,kwenda kinyume na maadili,utovu wa nidhamu na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Serikali.
Aidha,amewaagiza maafisa elimu ya Msingi na Sekondari,kufuata na kuzingatia sheria wanapohamisha watumishi kutoka sehemu moja kwenda nyingine kuhakikisha wanalipa stahiki za mtumishi wao ili kuepusha usumbufu kwa watumishi.
Alieleza kuwa,Serikali imeshaanza kuzifanyia kazi changamoto za walimu ikiwemo upandishaji wa madaraja ya mseleleko,kuboresha miundombinu ya shule,ujenzi wa nyumba za walimu na vifaa vya kufundishia ili kuinua kiwango cha taaluma mashuleni.
Katibu wa Chama cha Walimu Wilaya ya Namtumbo Deograsias Haule alisema, Chama hicho kina walimu 1,292 kati yao 1,265 sawa na asilimia 98 ni wanachama na matarajio kuona walimu asilimia 100 wanakuwa wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania.
Haule,amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuaminiwa kupeperusha Bendera ya Chama cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu na Mgombea Mwenza Dkt Emmanuel Nchimbi.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa namna inavyoshirikiana na Chama cha Walimu katika kuleta mafanikio chanya kwa walimu na sekta ya elimu ikiwemo kuruhusu walimu kupandishwa madaraja kwa wakati,kupata daraja la mseleleko na walimu kubadilishia muundo baada ya kujiendeleza.
Kwa mujibu wa Haule,licha ya mafanikio hayo lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile suala la kikokotoo kwani wastaafu wanapomaliza muda wao kwenye utumishi wa umma wanapokea fedha kidogo ambayo haikidhi kujikimu.
Ametaja changamoto nyingine ni nyumba za walimu kwani zilizopo ni chache na hata za kupanga hazipo,jambo linalopelekea kutafuta makazi mbali na eneo la kazi.
Katika hatua nyingine,chama hicho kimefanya uchaguzi wa viongozi mbalimbali watakaoongoza katika kipindi cha miaka mitano ambapo Mwalimu Jacob Mbunda,amechaguliwa kuwa mwenyekiti baada ya kupata kura 66 na kumbwaga mwenyekiti wa zamani Anna Mbawala aliyepata kura 35.