Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Vienna, Mhe. Naimi Sweetie Hamza Aziz ameshiriki Hafla ya Makabidhiano ya fedha za msaada wa Dola za Marekani milioni 4.8 zilizotolewa na UNIDO kutekeleza mradi wa kutengeneza betri za umeme (Lithium-ion) kwa ajili ya pikipiki na bajaj za usafirishaji nchini Tanzania.
Akikabidhi msaada huo Machi 25, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO. Bw. Gerd Müller, ameipongeza Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi tano za kwanza kunufaika na Mfuko wa Accelerate-to-Demonstrate chini ya UNIDO ulioanzishwa kwa ajili ya kusaidia mataifa mbalimbali katika jitihada za kuwa na nishati safi. Nchi nyingine zilizonufaika ni Kenya, Nigeria, Nepal, na Namibia.
Naye Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa, Vienna, Mhe. Lindsay Samantha Skoll alieleza kuwa, kutokana na umuhimu wa nishati safi katika maendeleo, Uingereza imechangia Pauni za Uingereza milioni 66 ili kusaidia utekelezaji wa miradi ya nishati safi hususan kwenye nchi zinazoendelea. Aidha, alieleza dhamira ya Uingereza kuendelea kusaidia jitihada za nchi mbalimbali kufikia malengo ya matumizi ya nishati safi. Balozi huyo pia alieleza kuwa, Uingereza inatarajia kuwa, fedha hizo zitatekeleza miradi iliyokusudiwa na kuleta matokeo chanya katika jamii.
Mhe. Balozi Naimi Aziz aliishukuru UNIDO na Serikali ya Uingereza kwa msaada huo na kueleza kuwa, mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya OASIS Financial Services Ltd ya Tanzania utasaidia kuongeza wigo wa matumizi ya nishati safi (clean energy) na kulinda mazingira, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuingiza betri za umeme nchini, kupunguza gharama za uendeshaji wa pikipiki na bajaj, uhaulishaji wa teknolojia, na kuzalisha ajira nchini.
Katika Hafla ya Makabidhiano hayo, ujumbe wa Kampuni ya OASIS Group uliongozwa na Bw. Stambuli Myovela, Afisa Mtendaji Mkuu na Mwanzilishi wa Kampuni hiyo.