FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imeandaa futari maalum kwa Wanajumuiya wa Kiislamu wa Chuo hicho ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano na mahusiano bora kati ya wafanyakazi na wanafunzi.
Hafla hiyo, imefanyika Katika Kampasi Kuu ya Edward Moringe iliyopo Manispaa ya Morogoro ilihudhuriwa na viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Morogoro, wanafunzi, na wafanyakazi wa SUA.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu SUA, Prof. Raphael Chibunda, aliwasihi Waislamu kuendeleza matendo mema hata baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Nawaomba msichoke kufanya mema kwa kuwa mwezi wa Ramadhani si kipindi cha muda mfupi bali ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Umoja na mshikamano ni mambo muhimu katika jamii,” alisema Prof. Chibunda.
Naye mwakilishi wa BAKWATA Mkoa wa Morogoro, Bw. Hafidhi Hussein, aliwahimiza Waislamu na wasio Waislamu kuthamini elimu kama nguzo muhimu ya maendeleo.
Hafla hiyo ilimalizika kwa waumini wa Kiislamu kufuturu pamoja, jambo lililochochea mshikamano na mahusiano mazuri ndani ya chuo hicho.