Na Prisca Libaga, Arumeru
Mkuu wa wilaya ya Arumeru Amir Mkalipa amewataka wananchi wa wilaya hiyo kutumia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katatua migogoro na malalamiko yao yanayosababishwa na kukosekana elimu ya msaada wa kisheria ili haki iweze kupatikana.
Mkalipa ameyasema hayo leo tarehe 31 Machi, 2025 wakati alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt Damas Ndumbaro wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyozinduliwa katika kata ya Makiba wilayani Arumeru.
Amesema Rais Samia anastahili pongezi kubwa kwa kuja na wazo la kuanzisha kampeni hiyo ambayo inakwenda kutatua migogoro mingi ya kisheria ambayo wao kama watawala wamekuwa wakishindwa kuitatua.
” Unajua sisi kama watawala linapokuja suala la mahakama tunashindwa kuingilia kati lakini kampeni hii ina wataalam wa sheria ambao wao ndio wamekuwa wakishinda mahakamani, wamekuja kumaliza kero hizo za wananchi watawaelekeza nini cha kufanya na mwisho kila mwananchi atapata haki yake,” amesema Mkalipa.
Amesema ijapokuwa siku kumi za kusikiliza kero za kisheria wilayani humo ni chache, lakini sio haba kwa kuwa sehemu kubwa ya migogoro itapatiwa ufumbuzi na wananchi watapunguza kufika ofisi za wilaya.
Wakiwasilisha migogoro yao mbele ya Mkuu wa Wilaya wananchi wa kijiji cha Malula wamelalamikia kutaka kupokonywa mashamba ambayo wamekuwa wakiyalima tangu mwaka 1972.
Wananchi hao wamemtaja mwananchi mmoja kwa jina la Zara kuwakataza kulima mashamba hayo akidai yeye ndio mmiliki wa mashamba hayo tangu miaka ya 1960 akiyarithi kutoka kwa marehemu wazazj wake.
Mkuu wa Wilaya Amir Mkalipa aliwaeleza wananchi hao kuwa mgogoro huo anaufahamu vizuri na kwamba mashamba hayo ni mali ya Serikali na imeshayatenga kwaajili ya eneo la uwekezaji (EPZ), na kwamba hakuna mtu yoyote aliyemilikishwa.
” Mashamba ya malula ni eneo la Serikali, yameshatengwa kwaajili ya uwekezaji wa EPZ lakini kama Serikali tutakuja kuwasikiliza na tutawapanga kwa muda ili muendelee kuyalima lakini sio kuwamiliķisha na watu wachache waliojenga nyumba zao zinaenda kubomolewa,”Amesema DC Mkalipa.
Kwa upande wake mkurugenzi wa huduma za msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Ester Msambazi amesema kuwa, Kampeni hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma za mawakili bure pamoja na elimu ya maswala ya kisheria.



