Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma(Mbifacu)Micheal Kanduyu kulia na Kaimu Meneja wa Chama hicho Faraja Komba wakiangalia uzalishaji wa zao la kahawa katika kijiji cha Malindindo Wilayani humo.
Miongoni mwa mashamba bora ya kahawa katika Mkoa wa Ruvuma.
Shamba la Kahawa katika kijiji cha Malindindo Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma likiwa linaendelea vizuri baada ya kuweka mbolea ya ruzuku.
………………
Na Mwandishi Maalum, Mbinga
WAKULIMA wa zao la Kahawa katika kijiji cha Malindindo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa mbolea za ruzuku zilizowawezesha kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo na kupata bei nzuri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakulima hao walisema,katika kipindi cha miaka minne cha Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan wamepata mafanikio makubwa ikilinganisha na miaka ya nyuma ambapo uzalishaji ulishuka kutokana na mbolea kuuzwa kwa bei kubwa na kahawa kuuzwa kwa bei ndogo hali isiyolingana na gharama za uzalishaji.
Hurban Mahai alisema,chini ya Serikali ya awamu ya sita wakulima wengi wamehamasika kufufua mashamba ya zamani waliyoyatelekeza na wengine kuanzisha mashamba mapya baada ya Serikali kuanza kutoa mbolea za ruzuku zinazouzwa kupitia mawakala na Vyama vya Ushirika kwa bei rahisi.
Mkulima mwingine wa kijiji hicho Donalt Nzuyu alisema,awali alikuwa anazalisha kati ya gunia 3 hadi 5 kwa ekari mojalakini kupitia mfumo wa mbolea za ruzuku ulioletwa na Serikali anazalishaji gunia 20 hadi 25.
Aidha alisema, miaka ya nyuma bei ya kahawa ilikuwa ndogo kwani kilo moja iliuzwa Sh.4,000 hivyo kuwakatisha tamaa wakulima ambao waliamua kuacha kulima zao hilo na badala yake kujikita kwenye mazao mengine yakiwemo mahindi na maharage.
Alisema,kutokana na mbolea za ruzuku kupatikana kirahisi sasa wanazalisha kwa wingi na mashamba yao yanapendeza na kuongezeka na amepongeza Viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilayani humo(Mbifacu)usimamizi mzuri wa mbolea hizo kwa wakulima kwani miaka ya nyuma waliteseka kutafuta pembejeo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Mbinga(Mbifacu)Micheal Kanduyu alisema,kupitia mfumo wa ruzuku mbolea ya UREA inauzwa Sh.68,000,CAN Sh.62,000 na SA inauzwa Sh.48,000.
Alisema,bei hiyo imewawezesha wakulima kuimudu hata akiuza kuku tofauti na awali ambapo bei ya mfuko mmoja ilikuwa Sh.150,000 hadi 180,000.
Kanduyu, ameiomba Serikali kuboresha soko la kahawa kwa kutafuta wanunuzi wengi zaidi kuja kununua kahawa kwa bei nzuri na kuendelea na utaratibu wa kutoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima wa zao hilo.
Kaimu Meneja wa Mbifacu Faraja Komba,ameishukuru Serikali kwa komo za madeni ya pembejeo kwa sababu linakwenda kuchavusha(kuongeza uzalishaji wa kahawa na kufikia lengo la Serikali la uzalishaji wa zao hilo ambapo Mkoa wa Ruvuma unatakiwa kuzalisha tani 300,000.
Komba alisema,katika kipindi cha miaka minne,uzalishaji wa kahawa katika Wilaya ya Mbinga umeongezeka kutoka tani 15,000 msimu 2022/2023 hadi tani 25,000 msimu 2024/2025.
Komba alisema,hayo ni mafanikio makubwa kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Serikali kwa ujumla kupitia Halmashauri za Wilaya ambazo kupitia ushuru zimefanikisha kukusanya zaidi ya Sh.bilioni 5.
Ametaja mafanikio mengine,ni matumizi sahihi ya pembejeo zilizopatikana kwa bei ya ruzuku na ameishukuru Serikali kwa kutoa pembejeo kwa bei ya punguzo ambapo Wakulima wameweza kupata mbolea za kutosha kwa ajili ya kuzalisha mazao kwenye mashamba yao.
Alisema,miaka ya nyuma pembejeo hususani mbolea iliuzwa kwa bei kubwa hivyo kusababisha wakulima wengi kushindwa kuendelea na kilimo cha zao hilo na wengine waliyatelekeza mashamba yao lakini sasa wakulima wamerudi tena shambani kwa kufufua mashamba baada ya Serikali ya awamu ya sita kuweka ruzuku kwenye mbolea.