*Ni Leseni Hodhi zilizorudi Serikalini baada ya kumalizika kesi na wawekezaji
*Mapato ya Serikali kuongezeka kupitia mrabaha na kodi mbalimbali
*Waziri Mavunde asisitiza kuongeza utafiti zaidi ili kuongeza uzalishaji wa dhahabu
*Wachimbaji wadogo nao wapatiwa Leseni kuongeza uzalishaji
Chunya- Mbeya
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amezindua rasmi shughuli za uchimbaji madini katika mgodi wa Porcupine North- uliopo Makongorosi Wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya unaomilikiwa na Kampuni ya Shanta Gold Mining Limited na kusema kuwa hatua hiyo ni matunda ya uamuzi wa Serikali kurudisha leseni ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha unawekwa utaratibu mzuri wa kuongeza mapato ya nchi kupitia sekta ya madini.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Aprili 03, 2025 katika hafla ya Uzinduzi wa Shughuli za Uchimbaji Madini Porcupine North – Kata ya Mkola, Makongorosi Wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya.
“Eneo hili ni eneo ambalo Leseni hodhi zimerudi serikalini kwa mujibu wa sheria. Baada ya kumalizika shauri la kimahakama na mwekezaji wa awali,serikali iliweka utaratibu wa wazi kumpata mwekezaji atakayeendesha eneo hili la uchimbaji na Kampuni ya Shanta Gold Mining Limited ilishinda kwa masharti ya kuanza uchimbaji ndani ya miezi 18,ambapo mashapo yaliyothibitishwa kwa sasa yanafikia wakia 110,000 na upo uwezekano baada ya utafiti zaidi kufikisha mashapo ya wakia 400,000 ambazo kupitia mrabaha,kodi na tozo mbalimbali zitasaidia kuongeza makusanyo ya Serikali” amesema Mavunde
Aidha, Waziri Mavunde amesema kuwa, Leseni moja iliyokuwa katika eneo la Saza, Mkoa wa Songwe, imekabidhi kwa wachimbaji wadogo ili kuhakikisha kundi hilo linanufaika na rasilimali za madini na kwamba eneo hilo la Saza lililokabidhiwa kwa Wachimbaji Wadogo, linakadiriwa kuwa na mashapo ya dhahabu yenye wakia laki mbili, thamani yake ikiwa ni takriban shilingi trilioni 1.2 kwa bei ya sasa ya dhahabu.
“Mgodi huu pia utatoa fursa za ajira kwa Watanzania, kuchangia maendeleo ya jamii kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) na kuhakikisha kunakuwepo na ushirikishwaji wa wazawa kupitia sera ya Local Content” Ameongeza Mavunde
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa tukio la uzinduzi wa shughuli za uchimbaji katika mgodi huo ni ushuhuda wa mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini Tanzania chini ya uongozi na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wasaidizi wake na kwa mgodi huo utakuwa mfano wa kipekee hapa nchini.
Wakizungumza kwa Nyakati tofauti, Mkuu wa Wilaya Chunya Alhaji Mbaraka Alhaji Mbaraka Batenga, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mbeya na Mkuu wa Wilaya ya Songwe Solomon Itunda, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Songwe wameleeza wamewapongeza wananchi wa Kata ya Mkola kwa kuruhusu hatua hiyo kufikiwa, kwa kutoa ushirikiano kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo vya kata hiyo na taifa kwa ujumla.
“Tunakupongeza wewe binafsi Mhe. Waziri Mavunde kwa kufuta leseni zilizokuwa hazifanyiwi kazi, ambazo baada ya kurudisha Serikalini mnaendelea kuwapanga vyema wachimbaji wadogo.” Amesisitiza Alhaj Batenga.
Nao, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Shanta Gold Mining Mhandisi Honest Mrema na Meneja wa Mgodi wa New Luika Gold Mine unaomilikiwa na Kampuni hiyo Mhandisi Exeuper Lyimo wametoa shukrani zao za dhati kwa Serikali kwa upatikanaji wa leseni hizo na hatimaye kuanza uchimbaji na uzalishaji.
“Kupitia Mgodi huu, Kampuni imeongeza uhai wa maisha ya Migodi yake hapa nchini kutoka mwaka 2031 hadi 2034 na kupitia utafiti tunaoendelea kufanya uhai wa migodi utaongezeka zaidi. Lakini pia, shughuli za uchimbaji madini katika mgodi huu zitafanywa na Kampuni za kitanzania kwa asilimia 100. Mgodi wa New Luika imeajiri wafanyakazi 1140 ambapo asilimia 40 ni wakazi wanaozunguka eneo la mradi na kuanza kwa mgodi huu kutasaidia kuongeza wafanyakazi zaidi ya 100 ambapo asilimia 60 yao ni vijana kutoka katika maeneo haya ya Porcupine.” Ameongeza Mhandisi Mrema.