Na. Mwandishi Wetu Baraka Venant- Kitulo.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limezindua Kampeni ya *vote now* ndani ya Hifadhi ya Taifa Kitulo yenye utajiri wa maua ya asili, leo Aprili 03, 2025 kwa lengo la kuwahamasisha watanzania kuzipigia kura Hifadhi za Taifa Kumi (10) zilizoingia katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo mbalimbali za utalii katika vipengele nane (8), tuzo zinazotolewa na taasisi ya World Travel Awards.
Akizindua kampeni hiyo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Jully Bede Lyimo – Mkuu wa Idara ya Utalii TANAPA kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA aliwasihi na kuwahamasisha watanzania kuzipigia kura hifadhi hizo ili zishinde na kunyakuwa tuzo hizo ili zitambulike zaidi kimataifa.
Kamishna Jully alisema, “Faida ya kushinda tuzo ni kuziweka hifadhi hizo kumi kwenye uso wa dunia kitu ambacho kitaongeza hamasa kwa watalii kutembelea hifadhi hizo na kuongeza pato kwa TANAPA na Taifa kwa ujumla.”
Aidha, Kamishna Jully aliongeza, “Kwa mwaka 2025 TANAPA kutokana na ubora wa hifadhi zake imeingiza hifadhi 10 kwa kategoria tofauti zikiwemo Hifadhi za Taifa Serengeti, Kilimanjaro, Nyerere, Tarangire, Ruaha, Katavi, Arusha, Milima ya Mahale na Udzungwa huku Hifadhi ya Taifa Kitulo inayosifika kwa maua mwitu ya aina tofauti ikiingia katika kinyang’anyiro cha Eneo bora zaidi Afrika la kufanyia fungate”.
Hata hivyo, Kamishna Jully alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizozifanya za kuitangaza Tanzania kupitia filamu mbili za “Royal Tour na The Amazing Tanzania” pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya uongozi wa Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana na Katibu Mkuu wake Dkt. Hassan Abbas.
Naye, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kitulo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Harry Gazi alisema kuwa hifadhi hiyo imestahili kuingia katika kinyang’anyiro kutokana na upekee wake na ubora wa spishi za maua aina ya Okidi zinapatikana maeneo machache sana duniani. Hivyo kuwania tuzo hiyo ni sahihi hususani kwa kipindi hicho cha fungate kwani maua ndio zana mbashara ya kuonyesha upendo wa wawili hao.
Hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo pia ilimjumuisha msanii wa kizazi kipya Mbwana Yusuph Kilungi (almaarufu Mbosso) ambaye kwa takribani miaka minne iliyopita aliwahi kurekodi wimbo wake ndani ya Hifadhi ya Taifa Kitulo na kuonyesha mazingira mazuri yaliyowapagawisha wafuasi wake.
Mbosso alisema, “Nimefarijika sana kujumuika kwenye kampeni hii kwani hifadhi hii naifahamu nilisharekodi wimbo wangu unaojulikana kama TAMU na nilipata “viewers” wengi na niliulizwa sana kuwa hapo ni wapi wengine wakahisi ni Ulaya. Hivyo hifadhi hii kuwekwa kwenye hicho kinyang’anyiro ni sahihi na niwaombe watanzania tuzipigie kura Hifadhi zote kumi za Taifa zishinde”.
Zoezi la kuzipigia kura hifadhi hizi lilishaanza hivyo uzinduzi wa kampeni hii umeihalalisha na tunahimizwa kwa wale ambao bado hawajapiga kura wazipigie kwani zoezi la upigaji kura unatarajiwa kutamatika Mei 04, 2025.