Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA Ashraph Yusuph Abdulkarim (kulia) akipokea zawadi ya ua toka Meneja Utawala na Rasilimaliwatu Mary Maridadi (kushoto) leo Aprili 04,2025 mara baada ya hafla ya kukabidhiwa rasmi ofisi kufuatia uteuzi wake uliofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Machi 25 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo Mhe. Hawa Ghasia akizungumza na watumishi leo Aprili 04,2025 wakati wa halfa ya makabidhiano ya ofisi za Shirika kwa Meneja Mkuu CPA Ashraph Yusuph Abdulkarim (hayupo pichani) ambapo amewataka watumishi kutoa ushirikiano kwa kiongozi huyo ili kutimiza malengo ya kuanzishwa kwa Shirika.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu toka Ofisi ya Rais TAMISEMI Emma Lyimo akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu OR-TAMISEMI wakati wa hafla ya kukabidhiwa Ofisi kwa Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA Ashraph Yusuph Abdulkarim (hayupo pichani) leo Apili 04 ,2025 jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja katika ya Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Masoko ya Kariakoo Mhe. Hawa Ghasia (aliyekaa katikati) pamoja na watumishi mara baada ya hafla ya makabidhiano ya Ofisi kwa Meneja Mkuu CPA Ashraph Yusuph Abdulkarim (aliyekaa kushoto) leo Aprili 04,2025 jijini Dar es Salaam.
Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA Ashraph Yusuph Abdulkarim akizungumza na watumishi mara baada ya kukabidhiwa ofisi hiyo leo Aprili 04,2025 jijini Dar es Salaam ambapo amewataka kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili kuleta tija. (Picha na Shirika la Masoko ya Kariakoo)
……
Watumishi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo wametakiwa kufanya mageuzi katika utendaji kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na taaluma walizonazo ili kufikia malengo ya Taasisi na kuongeza tija.
Hayo yamesemwa na Meneja Mkuu wa Shirika hilo, CPA Ashraph Yusuph Abdulkarim wakati alipozungumza kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika leo (Aprili 4,2025) Dar es Salaam.
Meneja Mkuu huyo alisema endapo watumishi watafanya kazi kwa nidhamu na uadilifu ni dhahiri kwamba uzalishaji utaongezeka na mazingira ya kazi yataboreshwa na kuleta ufanisi mzuri katika utendaji kazi wa Shirika.
“Nitashirikiana na watumishi wenzangu kulifanya Shirika lisonge mbele na kujiendesha kwa tija pamoja na kudhibiti uvujaji wa mapato, kuongeza vyanzo vya mapato na kuweka mipango mizuri ya kibiashara” alisema CPA Ashraph.
CPA Ashraph amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumteua kuongoza Shirika la Masoko ya Kariakoo kwa nafasi ya Meneja Mkuu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo Hawa Ghasia, pamoja na kumkaribisha Meneja Mkuu huyo alimwagiza kusimamia kwa ukaribu mchakato wa maandalizi ya ufunguzi wa soko la Kariakoo uliopangwa ukamilike mwezi huu Aprili.
“Kazi yako kubwa kwa sasa ni kuhakikisha soko la Kariakoo linafunguliwa mwezi huu Aprili ili kuwezesha wafanyabiashara waweze kuingia ndani kuendelea na biashara kufuatia mradi wa ujenzi na ukarabati wa soko kukamilika,” alisema Ghasia.
Ghasia alisisitiza kuwa Bodi ya Wakurugenzi ina imani kubwa na Mtendaji Mkuu huyo kutokana na uzoefu alioupata alipokuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hivyo aweke mipango ya kujenga masoko mengine maeneo ya Shirika ya Mbezi Beach na Tabata Bima.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Emma Lyimo aliyemwakilisha Katibu Mkuu kwenye hafla hiyo aliwasihi watumishi kutoa ushirikiano kwa Meneja Mkuu huyo ili atimize majukumu yake kwa ufasaha na kusaidia Shirika kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.