…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wametoa mafunzo ya usawa katika uongozi na biashara kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, kituo cha Tegeta ili kuwasaidia kujimudu katika nyanja mbalimbali hasa katika nafasi ya uongozi unaozingatia uwasa wa kijinsia mahali pa kazi.
Akizungumza leo April 4, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akitoa mafunzo kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Bi. Imelda Lutebinga, amesema kuwa ni muhimu kutoa elimu kwa wanafunzi ikiwa ni sehemu ya kupanda mbegu itakayosaidia Taifa.
Lutebinga, amesema kuwa mafunzo ya usawa katika uongozi na biashara ni rafiki kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwani yamegusa nyanya tofauti ikiwemo namna bora ya kuanzisha biashara pamoja na kutoa fursa ya kupata nyenzo itakayowasaidia baada ya kumaliza masomo yao.
“Nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe miaka 15 iliyopita na sasa nimepata fursa ya kushiriki katika nafasi ya maamuzi katika maeneo tofauti ili kulisaidia Taifa katika kuendeleza dira” amesema Lutebinga.
Lutebinga amesema kuwa ATE imekuwa na utamaduni wa kuendesha programu mbalimbali nchini ikiwemo kuwajengea uwezo wanawake kulingana na uhitaji hasa katika nafasi ya uongozi.
Amefafanua kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kutoa elimu kwa wahitimu zaidi ya 600 katika Serikali ya Tanzania Bara na mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema kuwa wanaendelea kutoa elimu ya mafunzo mbalimbali katika jamii ikiwemo kujiamini, kujieleza kwa ufasaha ili kuhakikisha wanawake wanakuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza katika nafasi yoyote ya uongozi.
Katika mafunzo hayo kulikuwa na watoa mada kutoka Taasisi mbalimbali ikiwemo Taasisi za biashara kutoka nchini Norway, Chuo Kikuu Mzumbe pamoja na Tanzania Startup Association ambapo wamesisitiza umuhimu wa wanafunzi kuwa na subira pamoja na kutengeneza mahusiano mazuri na wadau ili kufikia fursa kwa haraka baada ya kumaliza masomo.