Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, amewahimiza wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kufuata huduma za msaada wa kisheria zitakazotolewa katika halmashauri zote za Mkoa wa Tanga.
Huduma hizo ni sehemu ya kampeni ya kitaifa iliyoanzishwa na Rais Samia, ambayo tayari imeshafanyika katika mikoa 23 nchini.
ambapo katika kampeni hiyo, zaidi ya wananchi mil. 2 wamepatiwa msaada wa kisheria huku migogoro mbalimbali, ikiwemo ya ardhi, ikiwa imetatuliwa.
Akizungumza kuhusu kampeni hiyo, Dkt. Burian alisema katika, Mkoa wa Tanga,kampeni hiyo itazinduliwa rasmi Aprili 8, 2025 katika viwanja vya Tangamano, na baadaye itaendelea katika ngazi ya kata, vijiji na mitaa.
“Lengo kubwa la kampeni hii ni kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria na haki za binadamu ili jamii iweze kutambua haki zao na namna ya kuzitetea,” amesema RC Burian.
Kwa upande wake, Ofisa Uchunguzi Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na Mratibu wa Kampeni hiyo kwa Mkoa wa Tanga, Laurent Buliro, amesema kampeni hiyo itaendeshwa na maofisa wa kada mbalimbali wakiwemo wasaidizi wa kisheria, ambao wataunda timu moja katika kila Halmashauri.
“Majukumu yao yatakuwa ni kutoa elimu ya kisheria na haki za binadamu kwa wananchi, lakini pia tutafika katika shule za msingi na sekondari kutoa elimu kuhusu haki za binadamu na ukatili wa kijinsia,” amesema Buliro.