Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge.
……………..
Bohari ya Dawa (MSD) imenunua na kupeleka mashine za kisasa zenye Tekinolojia ya akili mnembo (Artificial Intelligence) kwa ajili ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ili kuiwezesha taasisi hiyo kutoa huduma za kisasa.
Mashine hizo ambazo baadhi tayari zimefungwa zinatarajia kuanza kutoa huduma muda wowote kuanzia sasa.
Akizungumza baada ya kupokea mashine hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge ameipongeza MSD kwa juhudi zake za kuhakikisha huduma za moyo zinakuwa za kisasa kwenye hospitali hiyo. “
Dkt. Kisenge ameishukuru MSD kwa kuleta mashine hizi ambazo zitasaidia kutoa huduma za moyo kwa ufanisi kwani mashine hizi zinauwezo wa kupiga picha sahihi kwa ajili ya matibabu lakini pia mashine hizi zinauwezo wa kutafsiri taarifa mbalimbali zenyewe kwa kutumia tekinolojia za kisasa.
Kwa upande mwingine Dkt. Kisenge, ameipongeza Bohari ya Dawa (MSD) kwa juhudi zake za kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa vya kisasa vya afya kwa haraka, jambo linaloimarisha huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo. “Tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na MSD katika kuhakikisha dawa na vifaa vya kisasa vinapatikana kwa haraka na kwa ufanisi,” alisema Dkt. Kisenge.
Amesema kuwa kwa sasa, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inahudumia zaidi ya wagonjwa elfu moja, na zaidi ya asilimia 95 ya wagonjwa hao wanapata vipimo na matibabu kwa kutumia vifaa vya kisasa ambavyo MSD imevinunua na kuvisambaza. Vifaa hivi vikiwemo mashine za kisasa za ECG (Electrocardiogram), na vifaa vya upasuaji wa moyo vinavyowezesha kutoa matibabu bora na ya haraka.
Naye Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam Bi. Betia Kaema amesema JKCI ni moja ya hospitali maalumu hivyo wanahakikisha huduma wanazowapa zinakuwa na ubora wa hali ya juu na kwa haraka kuanzia pale wanapopokea maombi yao, kuwa na vikao endelevu na vya mara kwa mara ili kuhakikisha huduma zinakuwepo muda wote na changamoto zote zinatatuliwa kwa wakati.
Vifaa hivyo ambavyo vimekabidhiwa vinagharimu jumla ya shilingi milioni 800.