Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Crispin Chalamila, leo Aprili 10,2025 hapa Jijini Dodoma wakati akifungua warsha kwa viongozi wa taasisi zinazohusika na uchaguzi na lengo la warsha hiyo inalenga kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia rushwa wakati wa uchaguzi.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Crispin Chalamila, amesema rushwa katika uchaguzi inaweza kudhoofisha utawala bora na demokrasia, ambapo baadhi ya wananchi wenye sifa za uongozi bora (mfano uadilifu na uwajibikaji) hushindwa kugombea au kutoteuliwa ama kutochaguliwa kwa kutokuwa tayari kutoa hongo.
Chalamila ameyasema hayo leo Aprili 10,2025 hapa Jijini Dodoma wakati akifungua warsha kwa viongozi wa taasisi zinazohusika na uchaguzi, n kuongeza kuwa warsha hiyo inalenga kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia rushwa wakati wa uchaguzi.
“Ni ukweli usiopingika kuwa rushwa katika uchaguzi ni sumu inayoharibu misingi ya demokrasia na utawala bora, na inapotokea, huathiri uchaguzi kwa njia mbalimbali,”amesema.
Adha, amesema warsha hiyo imeandaliwa kwa kutambua kuwa uchaguzi huru na wa haki hauwezi kuwepo bila ushiriki wa pamoja wa taasisi za serikali, kila moja ikitimiza wajibu wake kikamilifu na kwa mujibu wa sheria, weledi, uwazi na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Ameongeza kuwa vitendo vya rushwa katika uchaguzi ni moja ya vikwazo vya kutokuwa na uchaguzi unaozingatia misingi ya haki na usawa, na vinavyoathiri haki na fursa ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.
“TAKUKURU inaamini kuwa kwa kushirikiana baina ya taasisi hizi na kuchukua hatua stahiki kwa haraka, ndipo mafanikio katika kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi yatapatikana,” amesema.
Pia, ameongeza kuwa rushwa husababisha uvunjifu wa amani kutokana na migogoro ya mara kwa mara, na kuifanya nchi kugubikwa na vitendo vya rushwa vinavyosababisha baadhi ya wananchi kupoteza imani na mifumo ya taasisi na serikali, na hatimaye kuchangia machafuko.
Sanjari na hilo amesisitiza kuwa ni wajibu wa watumishi wa umma na taasisi za serikali zinazoshiriki katika mchakato wa uchaguzi kuhakikisha kwamba wanapanga na kutekeleza mikakati ya kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa.
“Ili kuzuia vitendo hivyo, taasisi hizo zina wajibu wa kuhakikisha uteuzi wa wagombea unazingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na usawa wa fursa, kuzuia matumizi mabaya ya rasilimali za umma, kudhibiti fedha za kampeni na kuhakikisha upatikanaji sawa wa fursa kwa vyama vya siasa na wagombea,”amesema.
Vilevile, kuhakikisha mazingira salama na ya haki bila vitisho wakati wa kupiga kura, na kuhakikisha ushughulikiaji wa malalamiko unafanyika kwa uwazi na haki, pamoja na kuchukua hatua dhidi ya watumishi na wanasiasa waliokiuka maadili.
Amesema warsha hiyo pia imelenga kujenga uelewa wa viashiria vya rushwa vinavyoambatana na uchaguzi, kubadilishana uzoefu na mbinu bora za kukabiliana na tatizo hilo wakati wa uchaguzi, na kuweka misingi ya ushirikiano baina ya taasisi hizo.
Ameeleza kuwa mada zitakazojadiliwa ni pamoja na namna ya kutambua mianya ya rushwa katika uchaguzi, na namna ya kudhibiti vitendo vya rushwa kabla na baada ya uchaguzi.