Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Said Yakubu amekutana na kufanya mazungumzo na Bi Kanizat Ibrahim ambaye ni Mjumbe wa Afrika katika Baraza la Uongozi la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ambaye ni raia wa Comoro.
Balozi Yakubu ametumia fursa hiyo kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake katika nafasi hiyo, na pia kumueleza namna soka la Tanzania linavyokua kwa kasi katika kipindi hichi cha urais wa Ndg. Wallace Karia hususan soka la wanawake na vilabu vikuu nchini vya Simba na Yanga.
Balozi Yakubu alimueleza Bi Kanizat kuwa, Serikali ya Tanzania imefanya juhudi kubwa kwa maendeleo ya soka ikiwemo uendelezaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa viwanja vipya na ukarabati wa vilivyopo, uenyeji wa mikutano mikubwa ya mashirikisho ya soka, uenyeji wa mashindano makubwa na pia kutoa fedha kwa timu za Taifa.
Kwa upande wake Bi Kanizat alieleza namna anavyopendezwa na maendeleo ya soka ya Tanzania na kuahidi kuisemea Afrika na Tanzania katika FIFA.