Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Mhe.Ridhiwani Kikwete, akizungumza na Waandishi wa habari leo Aprili 23,2025 jijini Dodoma kuelekea siku ya Maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani yanatarajia kufanyika Mkoani Singida Aprili 28 mwaka huu.
Sehemu ya waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Mhe.Ridhiwani Kikwete,(hayupo pichani) wakati akizungumza leo Aprili 23,2025 jijini Dodoma kuelekea siku ya Maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani yanatarajia kufanyika Mkoani Singida Aprili 28 mwaka huu.
Na.Alex Sonna-DODOMA
MAADHIMISHO Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani yanatarajia kufanyika Mkoani Singida Aprili 28 mwaka huu ambapo yataambatana na maonesho pamoja na wadau wengine ili kutoa elimu kwa umma na kubadilishana uzoefu miongoni mwao juu ya masuala ya usalama.
Hayo yamesema leo Aprili 23,2025 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Mhe.Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza na Waandishi wa habari ambapo amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha na uwekaji wa mazingira salama mahali pa kazi.
” Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wanaendesha kampeni maalum za uhamasishaji kupitia shughuli mbalimbali yakiwamo mafunzo ya usalama na afya miongoni mwa makundi mbalimbali yakiwemo wajasiliamali wadogo na watu wenye ulemavu”amesema Mhe.Kikwete
Amesema kuwa Maonesho haya yatafanyika viwanja vya Mandewa -Singida ambapo pia Kutakuwa na kliniki ya uchunguzi wa afya za wafanyakazi kwenye magonjwa ya wanawake, afya ya akili, sukari, saratani na macho.
Aidha Waziri Kikwete amesema siku hiyo pamoja na mambo mengine itaadhimishwa kwa kauli mbiu ya “nafasi ya akili mnemba na Teknolojia za kidigitali katika mapinduzi ya usalama na afya kazini”ikiwa imelenga kuhamasisha na kuwakumbusha waajiri kujiandaa kutumia akili mnemba katika uzalishaji na utoaji bora wa huduma.
” Teknolojia hii inaenda kuleta mabadiliko chanya ikiwemo machine na mifumo inayotumia akili mnemba kufanya kazi haraka,kwa usahihi bila kuchoka,ni vyema pia kutambua kuwa matumizi hayo hayamaanishi kupoteza ajira bali kuleta mabadiliko katika ajira, “amesema Mhe.Kikwete
Aidha amesema kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yataongeza mahitaji ya wataalam, mafundi wa mitambo ya kisasa na wasimamizi wa taarifa na mifumo ya akili mnemba.