Na Silivia Amandius.
Kyerwa, Kagera.
Zaidi ya wanafunzi 3,500, wakiwemo wenye mahitaji maalum, wamefaidika na kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Suluhu Hassan katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa. Kampeni hiyo imetekelezwa katika shule mbalimbali zikiwemo Shule ya Sekondari Mabira, Chanyangabwa, Nyabishenge, Nyakake pamoja na Shule ya Msingi Nyakatabe.
Kupitia kampeni hiyo, wanafunzi wamepata elimu juu ya namna ya kujikinga na ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, wameeleza kuwa licha ya serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu, bado wazazi wengi hawajawa na mwamko wa kutosha katika kuwapeleka watoto shule na kushiriki katika kuchangia huduma muhimu kama chakula shuleni.
Sadia Merchades Cosma, mwanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Mabira, ameeleza kuwa licha ya elimu inayotolewa mara kwa mara, bado vitendo vya ukatili kwa watoto vinaendelea, ambapo baadhi ya wazazi wamekuwa chanzo kwa kushindwa kuwapatia watoto malezi bora na kuwanyima fursa ya elimu.
Kwa upande wake, Kelvin Dauson (12), aliyesitisha masomo katika darasa la nne katika Shule ya Msingi Chabruga iliyopo Kata ya Songambele kutokana na kukosa michango ya shule, ameishukuru kampeni hiyo kwa kuwaelimisha wazazi kuhusu umuhimu wa elimu. Kelvin ameeleza kuwa sasa anatamani kurudi shule kutokana na mwamko mpya wa wazazi wake waliopata elimu kupitia kampeni hiyo.
Kampeni hii imekuwa chachu ya mabadiliko kwa familia nyingi wilayani Kyerwa, ikilenga kulinda haki za watoto na kuongeza uelewa kuhusu wajibu wa jamii katika kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya msingi ya elimu na malezi bora.