Azindua Shule ya Sekondari Migungani, awataka wanafunzi kutunza miundombinu
Asema Serikali yajipanga kujenga mradi mkubwa wa umeme Monduli
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Monduli kwa jitihada zao za kutatua migogoro ya ardhi wilayani humo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kuwataka viongozi kutatua changamoto za wananchi katika maeneo yao.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo Aprili 23, 2025 wilayani Monduli, mkoani Arusha wakati akihutubia wananchi mara baada ya kuzindua Shule Mpya ya Sekondari ya Migungani iliyopo wilayani humo.
“Naomba kuwapongeza tena uongozi wa Wilaya ya Monduli kwa kuendelea kufanya kazi nzuri sana hapa wilayani kwa maslahi mapana ya wananchi wa Monduli. Nimejulishwa kuwa, mmefanya mengi mno ikiwemo utatuzi wa changamoto na migogoro ya ardhi hapa wilayani. Nimejulishwa kuwa sehemu kubwa ya changamoto hizi mmefanikiwa kuzitatua hongereni sana,” amesema Dkt. Biteko.
Ameipongeza pia kamati ya kutatua kero za wananchi inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya ikiwa na wataalamu mbalimbali ambayo imejiwekea utaratibu wa kupokea kero kutoka kwa wananchi na kuzipatia ufumbuzi, ambapo ameitaka pia iratibu zoezi la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya ardhi.
Akiwa shuleni hapo, Dkt. Biteko amewapongeza wananchi kwa kujenga shule hiyo ya Sekondari Migungani na kufikia asilimia 85 ya ujenzi huku Serikali ikichangia shilingi milioni 500.
“ Sote tunafahamu kuwa, elimu ni msingi mkubwa wa maendeleo. Sisi wana Monduli tayari tunayo shule yetu hii ambayo imeshakamilika. Hii ni miongoni mwa shule zilizopo Wilayani hapa ambazo zitaendelea kutupatia elimu kwa vijana wetu,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Shule hiyo itakuwa na uwezo wa kuwa na wananfunzi 400 na hivyo amewataka wanafunzi kutunza miundombinu sambamba na kujifunza kwa bidi ili wajiandae kuwa wazalendo na raia wema huku wakiwa na uwezo wa kutafuta majibu ya matatizo watakayokumbana nayo.
Kuhusu miradi ya umeme wilayani humo, amesema kuwa mwaka huu Serikali inatarajia kujenga mradi mkubwa wa umeme kwa lengo la kuuongezea nguvu umeme unaopatikana ili uweze kufika Loliondo na kusaidia wilaya hiyo kuwa na umeme wa uhakika.
Aidha, Dkt. Biteko amezungumzia maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano kwa kuwataka Watanzania kuenzi muungano huo kwa kujenga Taifa moja kwa kushikamana na kufanyakazi kwa pamoja kwa kushirikiana.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Festo Kiswaga amesema kuwa Wilaya hiyo ni tegemeo kwa Chama Cha Mapinduzi na wamekuwa wakishirikiana na wananchi katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.
Pia, amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo barabara, hospitali, shule na kuwa Wilaya hiyo ni kati ya wilaya zinazofanya vizuri katika elimu na huku akimshukuru Rais Samia kwa kuwekeza katika elimu nchini.