Na WMJJWM – Dodoma
KATIBU Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu amesema, jukumu la kuiokoa Jamii na ukatili wa kijiinsia ni la kila mmoja hivyo ameiasa Jamii kushirikiana katika kupambana na vitendo hivyo.
Dkt. Jingu ameyasema hayo jijini Dodoma Aprili 23, 2025 wakati akiongoza kikao cha Kamati Tendaji ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024.
Dkt. Jingu ameeleza kuwa, licha ya mafanikio yanayoendelea kushuhudiwa kama vile kuimarika kwa huduma kwa waathirika wa ukatili na kuongezeka kwa uelewa wa jamii, bado kuna changamoto kubwa zinazohitaji kushughulikiwa kwa haraka na umakini.
“Changamoto kama umasikini wa kaya, ndoa na mimba za utotoni, ukatili wa kingono na kisaikolojia bado ni tatizo kubwa. Tunahitaji ushirikiano wa kweli baina ya sekta zote ili kuhakikisha MTAKUWWA inatekelezwa kikamilifu,” amesema Dkt. Jingu.
Dkt. Jingu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, asasi za kiraia na Taasisi nyingine kuhakikisha lengo la kupunguza ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 linafikiwa.
Naye Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dkt. Nandera Mhando, amewataka washiriki kwenda kusimamia vizuri majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuzingatia maelekezo na majumuisho ya kikao hicho ili kutekeleza na kufikia malengo ya MTAKUWWA ya kutokomeza ukatili, kwani utekelezaji thabiti wa mpango huu unahitaji dhamira ya dhati, uwajibikaji na usimamizi makini kutoka kwa kila mdau katika ngazi zote kuanzia Serikali Kuu hadi mitaani.
Aidha washiriki wa kikao hicho wamepongeza uongozi wa Wizara kwa mwelekeo mzuri katika kuratibu MTAKUWWA pamoja na uwasilishaji wa taarifa na majadiliano yenye tija, huku wakiahidi kwenda kutekeleza maelekezo yote kwa bidii, uwazi na ushirikiano ili kuhakikisha jitihada za kutokomeza ukatili zinazaa matunda katika jamii.