*Ailekeza TANESCO kufunga Kituo cha Kupoza Umeme Longido
*Maelekezo ya Serikali yatekelezwa Longido
*Amuagiza Makonda kusimamia ufungaji vifaa vya maabara Sekondari ya Longido Samia
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameeleza kufurahishwa kwake na ongezeko la ukusanyaji wa mapato katika kituo cha huduma za pamoja mpakani mwa Tanzania na Kenya cha Namanga.
Akizungumza leo Aprili 24, 2025 Namanga mkoani Arusha wakati katika ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano Dkt. Biteko ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania Kituo cha Namanga kwa kufanya kazi kwa ufanisi.
“ Nimefurahishwa sana na urahisi wa biashara na kila eneo limekuwa na ukuaji wa watu na bidhaa kwenye kusafirisha nje ya nchi ili kuleta fedha ya kigeni zitakazowezesha kufanya shughuli zingine nawapongeza sana, nawashukuru kwa kuwa na malengo makubwa ya kukusanya shilingi bilioni 124 na hadi kufikia leo mmekusanya shilingi bilioni 101 huku mkiwa na miezi kadhaa ya kuendelea kukusanya mapato” amesema Dkt. Biteko.
Amewataka watendaji hao kuendelea kuwa na utaratibu mzuri wa kurahisisha biashara kwa kuondosha mizigo inayosafirishwa kwa kutumia muda wa dakika 30 hadi 40 badala ya saa 2 kama ilivyokuwa hapo awali.
Ameendelea kusema kuwa Kituo hicho cha Namanga kilichofunguliwa mwaka 2018 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, hayati Dkt. John Pombe Magufuli na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta kwa lengo la kurahisisha biashara kati ya nchi hizo mbili. Hivyo, watendaji hao waendelee kuwa mabalozi wazuri kwa kutangaza taswira njema ya Tanzania wakati wakitekeleza majukumu yao.
Awali akikagua Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Longido Samia, Dkt. Biteko amesema kuwa baada ya siku kadhaa Kampuni ya Taifa Gesi itafunga miundo mbinu ya mfumo wa gesi shuleni ikiwa ni sehemu ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Pia, Dkt. Biteko amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda kuhakikisha Shule hiyo inapata vifaa vya maabara ili wanafunzi waweze kujifunza kwa vitendo na si nadharia pekee.
“ Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya hakikisheni hizi maabara zinafanya kazi kwa kupata vifaa, tabia ya wanafunzi kuchora bunsen bunner badala ya kuziiona na kuzitumia kwa kujifunzia kwa vitendo iishe, ” amesema Dkt. Biteko.
Amebainisha kuwa amemuelekeza Mkuu huyo wa Mkoa kuangalia namna ya kuweka uzio na kupata gari kwa ajili ya shule hiyo, huku akiwataka wanafunzi kujifunza kwa bidii ili watimize ndoto zao na kuwa Shule hiyo ni kielelezo cha Mkoa wa Arusha.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mundarara, Dkt. Biteko amesema madini ni kichocheo kikubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kuwa Kijiji cha Mundarara kimekuwa na uzalishaji wa madini ya rubi na kuwa anafurahishwa kwa kuona sasa Watanzania wanaweza kufanya kazi za uchimbaji wa madini.
Kuhusu umeme, Dkt. Biteko amesema “Vijiji vyote 52 vina umeme, kuna vitongoji 176 na vitongoji vyenye umeme ni 112 pekee. Kuna maeneo ambayo yanahitaji nguzo 25 na nimemuelekeza Meneja wa TANESCO ndani ya wiki tatu nguzo ziwekwe na watu wapate umeme. Nimemuelekeza pia Meneja na bosi wake transforma ije hapa wiki ijayo ifungwe na watu wapate umeme,” amesema Dkt. Biteko.
Vilevile, Dkt. Biteko ameelekeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kujenga njia nne za kupeleka umeme Loliondo, Namanga, Mundarara na Kamwanga na baadae kujenga kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme ili kusaidia wananchi kupata umeme na kufanya shughuli zao za kiuchumi.
Pamoja na hayo, amesema kuwa Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kuwaletea Watanzania maendeleo na kuwaasa wamuunge mkono. Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu kwa kuchagua viongozi watakao waletea maendeleo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amebainisha kuwa katika kusheherekea miaka 61 ya Muungano ni vyema kila Mtanzania ajiulize kwa nafasi yake, amefanya nini yeye binafsi, lakini pia amefanya kitu gani hasa cha kukumbukwa kwa watu wake wa karibu, kwa jamii inayomzunguka na pia kwa Taifa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Madini na Mbunge wa Longido, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kusaidia miradi ya maendeleo ambapo wachimbaji wadogo wilayani humo sasa wana umeme wa uhakika.
Ameendelea kusema Wilaya hiyo imenufaika na miradi ya maendeleo ambapo usanifu wa barabara ya kutoka Siha hadi Longido unaendelea.
“ Mgodi wa magadi soda wa Engaruka umetengewa fedha na tayari watu wako tayari kuja kuwekeza na itasaidia kujenga mji wa kisasa, tuna zaidi ya tani milioni 768 ambayo tunaweza kuchimba kwa muda mrefu bila kuisha. Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia wachimbaji wadogo wameweza kupata kiasi cha shilingi bilioni 9.999 ambapo Serikali inapata mapato, ”amesema Dkt. Kiruswa.
Amesisitiza “ Wilaya hii tumepewa fedha ya kujenga shule za sekondari sita katika kata zetu na tumebakiza kata tatu ambazo hazina shule za sekondari, kazi ya kujenga shule katika kata hizo inaendelea. Mafanikio haya yasingeweza bila kuwa na ushirikiano na mshikamano kati aya Chama Cha Mapinduzi, Serikali na viongozi wa kimila.”
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amesema kuwa maelekezo ya Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa kuhusu ujenzi wa daraja, upatikanaji wa haki na kituo cha afya yamefanyiwa kazi.
“ Tayari fedha zaidi ya shilingi milioni 250 imetolewa na baada ya wiki moja itaonekana kwenye mfumo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya. Kuhusu barabara, katika bajeti hii imetengwa fedha shilingi milioni 270, fedha hizi ni kwa ajili ya barabara ya Resingita yenye urefu wa km 13 na barabara ya Longido kwenda Meloe imetengewa shilingi milioni 105,”amesema Mhe. Makonda.