Dar es Salaam, Aprili 2025 — IDARA ya Uhamiaji nchini imetekeleza operesheni maalum ya ukaguzi wa raia wa kigeni kwa kipindi cha miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili 2025, ambapo jumla ya raia wa kigeni 7,069 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria za uhamiaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, SSI. Paul J. Mselle, operesheni hiyo ilifanyika katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na Kariakoo, lengo kuu likiwa ni kuwachukulia hatua za kisheria wale wanaoishi au kufanya kazi bila vibali halali au wanaokiuka masharti ya vibali vyao.
Kati ya waliokamatwa:
1,008 wamefikishwa mahakamani, ambapo 703 kati yao wamehukumiwa vifungo gerezani; 257 wamefanikiwa kuhalalisha ukaazi wao; 4,796 wameondoshwa nchini; Wengine 305 bado wanaendelea kufanyiwa uchunguzi.
Aidha, katika ukaguzi maalum uliofanyika eneo la Kariakoo, jumla ya raia wa kigeni 62 walikamatwa na kuondoshwa nchini kwa kosa la kuishi na kufanya biashara bila vibali halali, huku baadhi yao wakibainika kukiuka masharti ya vibali vyao vya biashara.
Idara ya Uhamiaji imetoa wito kwa raia wote wa kigeni wanaoishi au kufanya kazi nchini kuhakikisha wanazingatia masharti ya vibali vyao, ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria au usumbufu wowote wakati huu ambao zoezi la ukaguzi linaendelea nchini kote