Arusha .Benki ya CRDB imekabidhi hundi zenye thamani ya shilingi milioni 11 kwa washindi wa kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, inayofahamika kama ‘Panda Miti Usipande Fitina’, yenye lengo la kuhamasisha upandaji miti na utunzaji wa mazingira kwa viongozi wa mitaa, vijiji, vitongoji na mashina.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa CRDB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Sadat amesema,benki hiyo imeamua kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Mkoa katika kuboresha na kutunza mazingira kwa kutoa zawadi ya fedha kwa washindi wa mitaa, vijiji na vitongoji watakaofanya vizuri katika utunzaji wa mazingira na upandaji miti.
Ameongeza kuwa, “Tupo hapa kukabidhi hundi maalum kwa washindi wa kampeni ya mazingira. Tumekabidhi hundi mbalimbali kuanzia shilingi milioni tano, milioni mbili na milioni moja. Tumefanya hivi baada ya kupokea ombi la Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, na sisi kama benki tukaona ni jambo jema kushiriki kwa kuchangia sehemu ya faida tunayopata na kuirejesha kwa jamii.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema kuwa kampeni hiyo ni endelevu na itaendelea kufanyika kila baada ya miezi mitatu ili kuwatambua na kuwazawadia washindi wa mazingira.
Aidha Waziri Dkt. Doto Biteko amepongeza Benki ya CRDB kwa kushiriki katika kampeni hiyo pamoja na kumpongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuanzisha ubunifu wa kushindanisha mitaa, vijiji na vitongoji katika upandaji miti na utunzaji wa mazingira.
Amesema, “Lengo ni kuyaweka mazingira yetu katika hali ya usafi, hongereni sana!”
Miongoni mwa walionufaika na kampeni hiyo ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru na viongozi wa vijiji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC) na Arusha jiji.