MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imesema Mei 6,2025 itatoa uamuzi dhidi ya mapingamizi yaliyotolewa na upande wa utetezi baada ya kusikiliza majibu yaliyotolewa na upande wa Jamhuri juu ya kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Taifa Tundu Lissu kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
Katika mapingamizi hayo, upande wa utetezi wanataka mteja wao (Tundu Lissu) afikishwe mahakamani hapo huku mshtakiwa mwenyewe akisisitiza kuwa kesi hiyo iendeshwe kwa uwazi ili kila mmoja apate kufatilia kinachoendelea.
Wakati mshtakiwa akitaka hivyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Job Mrema umesisitiza kuomba kesi hiyo isikilizwe kwa njia ya mtandao na kwamba iahirishwe kwa siku 30 ili kuwapa nafasi utetezi kujiandaa na pia kuwapa fursa ya kuwasiliana na mteja wao.
Kadhalika Upande wa Jamhuri umepinga hoja ya utetezi kwamba mteja wao alifanyiwa ukiukwaji wa kisheria wakati akihamishwa gereza kutoka Keko Kwenda Ukonga akisema kwamba hapakuwa na ukiukwaji wowote wa kisheria na haki yake haikuathiriwa popote. Amesema Magereza ilitekeleza utaratibu wao na hawakuwa na amri ya wapi anapaswa kupelekwa hivyo Magereza walikua sahihi.
Pia Jamhuri wameiomba mahakama isitoe amri yotote ya kumita Mkuu wa Magereza la Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa gereza la Ukonga na maafisa wa magereza ambao hawakutajwa majina yao kama utetezi walivyoomba, kwa sababu mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza hoja zinazohusu Jeshi la Magereza.
Katika majumuisho wa hoja zao, Upande wa Jamhuri umeiombao Mahakama izingatie ombi lao la kuahirisha kesi hiyo kwa siku 30 lakini pia Mahakama ipuuze hoja za Utetezi na ikubaliane na tafsiri ya Upande wa Serikali kwamba Mahakama mtandao ni Mahakama ya wazi.
Wakijibu hoja za upande wa Jamhuri, Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili Mpare Mpoki wameendelea kusimamia hoja zao kwamba mteja wao aletwe Mahakamani na si kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya mtandao kwa kuwa inawatenga baadhi ya watu ambao hawana simu za kisasa yaani “Smartphone”
Akitoa hoja hiyo Wakili Mpoki amesema si wote watakua na uwezo wa kufuatilia kesi hiyo kwa njia ya mtandao lakini pia wapo wanaotegemea waandishi ambao nao wamezuiliwa kuingia mahakamani.
Utetezi wamejumuisha hoja zao kwa kuiomba Mahakama izingatie hoja zao na mteja wao afikishwe mahakamani na ipuuze hoja za Jamhuri.
Lissu alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Kisutu Aprili 10, 2025 akikabiliwa na kesi mbili moja ya uhaini na nyingine ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.
Kwa mujibu wa hati ya mahitaka, ilidaiwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam. Ilidaiwa kuwa Lissu akiwa ndani ya jiji la Dar es Salaam alitangeneza nia ya kushawishi au kuchochea umma ya kuweza kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania kwa kusema maneno yafuatayo;
“Walisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi tutahamasisha uasi, hiyo ndio namna ya kupata mabadiliko….kwa hiyo tunaenda kukinukisha sanasana huu uchaguzi tutaenda kuvuruga kwelikweli, tunaenda kukinukisha vibaya sana.”