WAZIRI wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde,akizungumza leo Aprili 30, 2025 jijini Dodoma kwenye ufunguzi wa kikao cha Menejimenti ya Tume ya Madini.
……
WAZIRI wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde (MB) ametoa maelekezo matano kwa Menejimenti ya Tume ya Madini hasa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuzingatia na kusimamia sheria katika utekelezaji wa majukumu yao na kufikiri nje ya boksi ili kuwa na kitu cha ziada katika kuendeleza Sekta ya Madini.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Aprili 30, 2025 jijini Dodoma kwenye ufunguzi wa kikao cha Menejimenti ya Tume ya Madini ambapo amewataka watendaji kuwa wabunifu katika maeneo yao, washirikiane, mkoa mmoja na mkoa mwingine pamoja na kushauriana.
“Kwenye Sekta ya Madini ukiweka sheria pembeni utaivuruga sekta, kuna wakati matumizi ya busara huwa yanahitajika lakini sheria kwanza, kaisimamieni, kesho keshokutwa mtu atakuuliza jambo lingine lolote dhamira yako ilikuwa nini na sheria inasema nini, kasimamie sheria kwanza na kama kuna maelekezo tofauti yasitokane na wewe, wewe katimize wajibu wako wa kusimamia sheria ni muhimu sana,”amesema Waziri Mavunde.
Agizo la pili ambalo amelitoa Mheshimiwa Mavunde ni kutaka ubunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
“Nataka mkawe wabunifu, tumenunua magari 101 mengine yanakuja pikipiki 140 Rais Daktari Samia Suluhu Hassan ametupatia nyenzo, nataka mfikiri nje ya boksi nini ufanye kwenye eneo lako ili sekta iweze kushamiri zaidi, isiwe ‘business as usual’ tunatamani kuona kila mtu katika eneo lake anajitahidi,”amesema.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Mavunde amewapongeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwa ukusanyaji wa maduhuli na kuwataka kutorudi nyuma na kuhakikisha kila mmoja anavuka lengo alilopangiwa na kuongeza kuwa,
“Mjitahidi kutafuta njia za kuongeza makusanyo pasipo kuleta athari kwa watu mnaowasimamia. Zipo njia nyingi za kufanya simamieni hilo, sisi tunaingiza fedha nyingi sana katika mfuko mkuu wa Serikali, miradi inayokuja mikubwa naamini tutafanya vizuri zaidi.
Katika agizo la nne la uadilifu Waziri Mavunde ameeleza kuwa hivi karibuni Sekta ya Madini imekuwa na utulivu pasipo kuwepo na malalamiko yoyote na kuwataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuendelea kutenda haki pasipo kuonea wadau wa madini na kutatua migororo na changamoto zinazowakumba wadau wa madini.
Amewasisitiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanatatua migogoro kwa kufuata haki ili kujenga imani na wachimbaji wa madini na kuendelea kutoa elimu kuhusu Sheria na Kanuni za Madini ili kupunguza migogoro kabisa.
Akitoa agizo la Tano Mheshimiwa Mavunde amesema kuwa ili kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini, imeundwa kamati maalum ya kuwajengea uwezo watanzania kushiriki kikamilifu katika Sekta ya Madini ili baadaye wawe wachimbaji wakubwa wa madini na kuelekeza Watendaji wa Tume ya Madini kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo.
“Wanapokuwepo wachimbaji wakubwa ambao ni wazawa faida lukuki zinapatikana ikiwa ni pamoja na ajira, mapato na ongezeko la manunuzi ya bidhaa na huduma za ndani ya nchi,” amesema Waziri Mavunde.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya uongezaji thamani madini nchini ambapo mpaka sasa wawekezaji wengi wamejitokeza kwenye ujenzi wa viwanda vya uongezaji thamani katika mikoa ya kimadini ya Chunya, Dodoma, Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Rukwa na Lindi.
Amesema kutokana na utendaji mzuri wa Sekta ya Madini hasa mchango wake kwenye Pato la Taifa kufikia asilimia 10.1 nchi ya Kenya kupitia Waziri wa Madini na Uchumi wa Bluu, Mheshimiwa Ali Hassan Joho wameomba kuja kujifunza nchini Tanzania.
Aidha, amewataka wachimbaji wa madini waliopewa leseni kuzifanyia kazi na kwa ambao hawajazifanyia kazi hatua mbalimbali za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuandikiwa hati za makosa na kufutwa kwa mujibu wa sheria.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba akizungumza katika mkutano huo amewataka Viongozi wa Tume ya Madini kuendelea kuimarisha upendo sambamba na kushirikiana ili Sekta ya Madini iendelee kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.
Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha akielezea hali ya makusanyo ya maduhuli katika Tume ya Madini amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 753.8 sawa na asilimia 85.45 ya lengo kilikusanywa.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 kuanzia mwezi Julai hadi Aprili 29, 2025 Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Bulioni 862.64 ambacho ni sawa na asilimia 86.53 ya lengo la Shilingi Trilioni Moja.
“Tunaamini kiasi kilichobaki tutakikamilisha ifikapo Juni, 30 mwaka huu kwa kuongeza nguvu na ubunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli na udhibiti wa mianya ya upotevu wa mapato,” amesisitiza Kamishna Mwasha.