Na John Mapepele
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameshiriki hafla ya utoaji wa Tuzo za Samia Kalamu Awards 2025 kwa Waandishi wa Habari iliyofanyika katika ukumbi wa The Super Dome Masaki Jijini Dar es Salaam tarehe 05 Mei, 2025.
Akiwa katika tukio hilo, Mhe. Mchengerwa ametoa tuzo kwa mtangazaji Leila Sanga wa Dodoma Fm Radio kituo ambacho kimeshinda tuzo ya kipengele cha redio za jamii.
Dodoma Fm Radio ni kituo kilichopo Dodoma, kilianzishwa mwaka 2010 kikiwa na lengo la kuchangia maendeleo ya mkoa wa Dodoma katika nyanja mbalimbali.
Makala iliyoshinda katika tuzo hizi inaitwa “Nani anaathirika na mabadiliko ya tabia nchi” ambapo iliangazia matumizi ya nishati safi yanavyoweza kuwapunguzia wanawake adha ya kufuata kuni umbali mrefu kitendo kinachowafanya kukutana na ukatili wa kijinsia ,pia matumizi ya nishati safi ya kupikia yanavyoweza kuokoa muda kwa mwanamke kufanya shughuli za kiuchumi.
“Tulifanya hivi kwa sababu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia
Pia kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi
Kuokoa wanawake na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa jamii ya Dodoma ambapo wanawake wengi wanalazimika kufuata kuni umbali mrefu”. Amefafanua Sanga
Mgeni rasmi katika tukio hilo amekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo alisistiza Waandishi wa Habari kuwa wazalendo kwa nchi yao wakati wanafanya kazi zao.
Aidha, amewataka kuelezea mafanikio na mageuzi yanayofanywa na Serikali.
Amevipongeza Vyombo vya Habari kwa kazi nzuri vinayofanya kwa kutangaza miradi mbalimbali ya Serikali.
“Ndugu zangu hatusemi kuwa msiikosoe Serikali bali tunasema tuwe wazalendo kwa nchi yetu kwa kuwa hatuna Tanzania nyingine” amesisitiza Mhe. Rais
Tuzo hizo ziliandaliwa na Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania na Mamlaka ya Mawasilino Tanzania ambapo tuzo katika sekta mbalimbali zilitolewa.