
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. David Cleopa Msuya, kilichotokea leo Mei 7, 2025, katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam, ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo.
Kupitia taarifa rasmi ya Ikulu, Rais Dkt. Samia ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa, kuanzia leo Mei 7 hadi Mei 13, 2025, ambapo bendera zote nchini zitapepea nusu mlingoti kwa heshima ya kiongozi huyo mkongwe aliyetoa mchango mkubwa katika historia ya taifa.
Rais Samia ametoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa msiba huu mzito, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa taarifa kamili kuhusu mipango ya mazishi kadri mipango inavyokamilika.
Mhe. Msuya anakumbukwa kwa utumishi wake wa muda mrefu serikalini, akiwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kabisa wa Serikali baada ya Uhuru, na akiwa Waziri Mkuu katika vipindi viwili tofauti. Mchango wake katika kujenga misingi ya utawala bora, uchumi na umoja wa kitaifa ni sehemu ya urithi mkubwa wa taifa.
Saa 24 inaungana na Watanzania wote katika kuomboleza msiba huu mkubwa.