Na Ashrack Miraji Fullshangwe
Same, Kilimanjaro – Katika mkutano wa wadau wa sekta ya madini uliofanyika leo katika Wilaya ya Same, Meneja wa Benki ya TCB (Tanzania Commercial Bank) tawi la Same, Mohamed Amri alitumia jukwaa hilo kutoa wito kwa wawekezaji wa madini kuchangamkia fursa za mikopo zinazotolewa na benki hiyo ili kukuza shughuli zao za uchimbaji na uongezaji thamani wa madini.
Alizungumza na washiriki wa mkutano huo, Meneja Amri alisema benki yake imejipanga kikamilifu kutoa huduma za kifedha zinazolenga kukuza uchumi wa ndani kupitia uwekezaji katika sekta ya madini. Alieleza kuwa TCB ina bidhaa mbalimbali za kifedha zinazowalenga wachimbaji wadogo na wa kati, pamoja na wawekezaji wakubwa katika sekta hiyo.
“Tunafahamu kuwa changamoto kubwa kwa wawekezaji wa madini ni upatikanaji wa mitaji. Hii ndiyo sababu TCB imekuja na mkakati mahususi wa kuwasogezea huduma hizi kwa urahisi ili kusaidia kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla,” alisema Meneja Mohamed Amri.
Aliwahimiza wawekezaji kutumia fursa ya mikutano kama hiyo kujifunza, kushirikiana na taasisi za kifedha kama TCB ambazo ziko tayari kusaidia kwa masharti nafuu. Aidha, aliwahakikishia kuwa benki yao ina utaalamu na uzoefu wa kuhudumia sekta hiyo kwa weledi mkubwa.
Wadau walioudhuria mkutano huo walipokea kwa shangwe wito huo, wakisema kuwa hatua hiyo itaongeza kasi ya maendeleo katika sekta ya madini hususan kwa wachimbaji wadogo wanaokosa mitaji ya kujiendeleza. Baadhi yao walieleza kuwa walikuwa hawajui kama TCB inatoa huduma maalum kwa wachimbaji wa madini.
Mkutano huo uliwakutanisha wachimbaji, wasambazaji wa vifaa vya uchimbaji, maafisa wa serikali, pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za kifedha. Mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwa ni pamoja na changamoto za kisheria, mazingira, na upatikanaji wa masoko ya madini.
Kwa kumalizia, Meneja Amri alitoa rai kwa viongozi wa serikali na wadau wengine kushirikiana kwa karibu na benki ili kuhakikisha kuwa wachimbaji wote wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu mikopo, ruzuku na huduma zingine za kifedha. Alisisitiza kuwa kwa ushirikiano, sekta ya madini inaweza kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi katika mikoa ya kaskazini na taifa kwa ujumla.