Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameungana na watanzania kuomboleza kifo cha mmoja wa waasisi wa tasnia ya habari nchini, Bw. Charles Hilary, ambaye hadi mauti yanamkuta alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu Zanzibar.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rais Samia ameonyesha kuguswa na msiba huo, akieleza kuwa amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Bw. Hilary kilichotokea leo Mei 11, 2025.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Bw. Charles Hilary… Ninatoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi, familia, ndugu, jamaa na marafiki, pamoja na wadau wote wa sekta ya habari nchini kwa msiba huu,” ameandika Rais Samia.
Ameongeza kuwa marehemu Hilary atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa zaidi ya miongo minne katika kukuza tasnia ya habari, kuanzia redio hadi televisheni, pamoja na kuwa mlezi na mshauri wa wanahabari chipukizi.
“Namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, na kuwapa familia yake nguvu na subira katika kipindi hiki kigumu,” ameandika Rais Samia, akihitimisha kwa maneno ya Qur’an: “Hakika sote ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake tutarejea.