NAIROBI, MEI 11, 2025 – KCB Leadership Centre
Katika usiku wa kuamkia leo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa Tuzo ya Heshima ya Juu kabisa kwa Kiongozi wa Kike Afrika Mashariki inayojulikana kama “The Historical Lifetime Achievement Award” katika tamasha la Thamani Awards 2025, lililofanyika katika Kituo cha Uongozi cha KCB, jijini Nairobi, Kenya.
Tuzo hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango ya Kiuchumi na Hazina ya Kenya, Dkt. Boniface Makokha, na kupokelewa kwa niaba ya Mheshimiwa Rais na wawakilishi wake, Dkt. Cassypool na Wellu Sengo.
Mkuu wa Sekretarieti ya Thamani Awards, Bi. Esther Wairimu Kiai, alitoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Samia kwa mafanikio yake makubwa katika uongozi na mchango wake wa kihistoria katika maendeleo ya jamii, utawala bora, na usawa wa kijinsia.
Waandalizi wa tuzo hizo wametangaza kuwa wana mpango wa kuandaa toleo lijalo la Thamani Awards nchini Tanzania mwaka ujao, Mungu akijalia.