Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Denice Simba, akizungumza katika kikaokazi kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, Jukwaa la Wahariri na PPRA kilichofanyika kwenye hoteli ya Jada Moroco Square jijini Dar es Salaam Mei 12, 2025.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina Sabato Kosuri akizungumza jambo na Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri TEF katika kikao hicho Bakari Machumu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina Sabato Kosuri akifafanua jambo katika kikao kazi hicho.
Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri TEF katika kikao hicho Bakari Machumu
…………..
Dar es Salaam, Mei 12, 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Denice Simba, amesema kuwa mahali popote panapohusisha matumizi ya fedha nyingi, ni lazima kuwe na usimamizi madhubuti ili kuhakikisha uwajibikaji kwa wote wanaotoa huduma au bidhaa katika taasisi za umma.
Bw. Simba aliyasema hayo leo wakati akifungua kikao kazi kati ya PPRA na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kufanyika katika Hoteli ya Jada, Morocco Square jijini Dar es Salaam.
Amesema utekelezaji mzuri wa ununuzi wa umma unahitaji kuwa na mamlaka madhubuti ya kusimamia watoa huduma pamoja na wanunuzi kutoka taasisi mbalimbali, ili shughuli hizo ziweze kufanyika kwa ufanisi na kuchochea maendeleo ya haraka.
“Ili kufanikisha hili, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeamua shughuli zote za ununuzi wa umma zifanyike kwa njia ya kidijitali kutokana na changamoto za mfumo wa kawaida wa manunuzi,” alisema Bw. Simba.
Ameongeza kuwa Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 imeipa PPRA mamlaka ya kusimamia mfumo wa ununuzi kwa njia ya mtandao (e-Procurement) ili kurahisisha na kuharakisha uchakataji wa zabuni zote za umma kupitia mfumo huo.
“Lengo kubwa ni kuboresha ununuzi wa umma kwa njia ya mtandao kwa kuongeza uwazi, kuzuia mianya ya rushwa, kupunguza gharama na muda wa mchakato, pamoja na kuimarisha ushiriki wa wazabuni wa ndani na nje ya nchi,” alieleza.
Kwa mujibu wa Simba, hadi kufikia sasa jumla ya wazabuni 33,470 wamesajiliwa katika mfumo huo. Tangu Aprili mwaka huu, mikataba na malipo yote ya ununuzi wa umma yameanza kufanyika ndani ya mfumo huo wa kidijitali.
Amebainisha kuwa jitihada zinaendelea kuimarisha mfumo huo kwa kuongeza moduli za ziada kama vile ukaguzi wa ndani na mfumo wa kupokea malalamiko kutoka kwa wazabuni, ambapo kwa sasa malalamiko yanashughulikiwa moja kwa moja kupitia mfumo kwa haraka na uwazi.
“Hadi kufikia Machi 2025, zaidi ya wazabuni 34,000 walikuwa tayari wamesajiliwa katika mfumo huu,” aliongeza.