Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Profesa Cyriacus Binamungu akizungumza na washiriki wa mafunzo kwa vitendo ya mfumo wa ofisi mtandao (E-OFFICE), Mfumo wa baruapepe (GMS) na uzingatiaji wa sheria ya matumizi sahihi ya mifumo tumizi ya tehama kwa taasisi za umma wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mkufunzi wa mafunzo ya mifumo tumizi ya serikali kitaifa ambaye pia ni Afisa TEHAMA Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe Bw. Alexander Benedicto akieleza lengo mafunzo kwa vitendo ya mfumo wa ofisi mtandao (E-OFFICE), Mfumo wa baruapepe (GMS) na uzingatiaji wa sheria ya matumizi sahihi ya mifumo tumizi ya tehama kwa taasisi za umma wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo kwa vitendo ya mfumo wa ofisi mtandao (E-OFFICE), Mfumo wa baruapepe (GMS) na uzingatiaji wa sheria ya matumizi sahihi ya mifumo tumizi ya tehama kwa taasisi za umma wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
………..
Chuo Kikuu Mzumbe chenye Mkataba wa Makubaliano na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wa kutoa mafunzo ya mifumo tumizi ya TEHAMA nchini kwa Taasisi za Umma, kimeendesha mafunzo kwa vitendo ya mfumo wa Ofisi Mtandao na Mfumo wa Barua pepe za Serikali kwa watumishi wa Umma kwa kada za Afisa Utumishi/Utawala, Afisa TEHAMA na Watumishi wa Masijala.
Mafunzo haya yanaendelea kwa awamu ya tatu yakijumuisha washiriki takribani 56 kutoka taasisi mbalimbali yatafanyika kwa siku tano kuanzia Mei 12 – 17, 2025, Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kituo cha Tegeta.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Prof. Cyriacus Binamungu amewapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwa kuona umuhimu wa kujifunza zaidi na kuwataka kwenda kutumia elimu hiyo kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi hasa katika dhama hizi za Sayansi na Teknolojia.
“Chuo Kikuu Mzumbe tunatoa huduma za mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa kada mbalimbali hivyo, tunajivunia kuwa na mkufunzi huyu aliyeaminiwa kitaifa, hivyo nitoe wito kwenu kutumia fursa hii ili kujifunza zaidi na kupata maarifa yatakayosaidia kuleta ufanisi katika taasisi zetu na Taifa kwa ujumla”. Alisema Prof. Binamungu.
Kwa upande wake mkufunzi wa mifumo tumizi ya Serikali kitaifa ambaye pia ni Afisa TEHAMA Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Alexander Benedicto ameeleza lengo la mafunzo haya ni kutoa uelewa wa mfumo kwa kina za moduli mpya zilizoongezwa kwenye Toleo la 5, Mfumo wa Barua pepe (GMS) na mafunzo ya Sheria ya Serikali Mtandao, Mwongozo wa Matumizi Sahihi wa TEHAMA kwa watumiaji wakuu na wasimamizi wa Mfumo huu kama matarajio ya Serikali.
Akitoa neno la Shukrani mmoja wa washiriki aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti wa mafunzo, Afisa Tawala Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Bw. Joel Junior Mkwizu ameipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa namna wanavyosimamia mifumo ya TEHAMA ya Serikali kwa watumishi wa Umma. Pia ametoa pongezi kwa Chuo Kikuu Mzumbe.