Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini kwa kushirikiana na Asasi ya Bluecross Society of Tanzania tarehe 13.05.2025 imetoa mafunzo maalumu kwa wazazi 47 juu ya madhara ya tatizo la dawa za kulevya katika Ukumbi wa Kanisa la Anglikana jijini Arusha.
Wazazi hao kutoka Shule 8 za Jiji la Arusha walielezewa mbinu za kumtambua mtoto ambaye ameshaanza kujihusisha na dawa za kulevya na jinsi ya kumuepusha na tatizo hilo. Pia walihimizwa umuhimu wa malezi bora katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya katika familia zao.
Wazazi hao walihamasishwa kuendelea kushirikiana na Mamlaka kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa hizo katika maeneo yao wanayoishi kwa kupiga namba ya simu ya bure ya 119.



