Na WAF – Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 bado ipo na inaendelea kutumika kutoa miongozo ya utoaji wa huduma za afya nchini, ikiwemo huduma ya bure kwa akinamama wajawazito.
Akijibu swali la Mhe.George Ranwell Mwenisongole (Mbunge wa Mbozi), leo Mei 16, 2025 Bungeni jijini Dodoma, aliyetaka kufahamu kama Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007, kuhusu akina mama wajawazito kujifungua bure kama bado inatumika.
Dkt. Mollel ameeleza kuwa licha ya sera hiyo kuendelea kutumika, Serikali kupitia Wizara ya Afya ipo katika hatua za mwisho za kufanya mapitio ya sera hiyo ili kuendana na mahitaji ya sasa ya afya.
“Huduma ya kujifungua bure bado ipo kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007. Hata hivyo, kuanza kutumika kwa Bima ya Afya kwa Wote kutakuwa suluhisho la kudumu katika kuhakikisha huduma bora na endelevu kwa mama na mtoto,” amesema Dkt. Mollel.
Serikali inasisitiza kuwa kupitia mfumo wa bima ya afya kwa wote, huduma zitaboreshwa zaidi huku wananchi wakipata huduma stahiki kwa wakati na bila vikwazo vya gharama.