Na Mwandishi Wetu – Kasulu
Katika Mahakama ya Wilaya ya Kasulu, Afisa Mtendaji wa Kata ya Rungwe Mpya, Bi. Tausi Issa Manyanya, amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Shauri hilo la jinai namba CC 11711/2025 lilisikilizwa tarehe 15 Mei 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mheshimiwa Emaculate Emanuel Shulli (RM). Mshtakiwa anakabiliwa na makosa mawili chini ya kifungu cha 15(1)(a) na 15(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2022.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, inadaiwa kuwa Bi. Manyanya alitenda makosa hayo akiwa katika kijiji cha Rungwe Mpya, Kata ya Rungwe Mpya, ambapo alidai na kupokea hongo ya shilingi 210,000 kutoka kwa mfugaji Bw. Omari Haruna, mkazi wa Kijiji cha Kigembe. Fedha hizo zilidaiwa kutolewa ili kuruhusu kurudishwa kwa ng’ombe mmoja wa Bw. Haruna aliyepotea na kupatikana katika kijiji hicho, ambapo alikuwa amehifadhiwa kwa mfugaji Longo Lugata Shija kwa maelekezo ya Afisa Mtendaji huyo.
Bi. Manyanya alikana mashtaka yote mawili yaliyosomwa mbele ya Mahakama na Waendesha Mashtaka wa Serikali kutoka TAKUKURU, Bw. James Mosi Nyarobi na Bw. Davis Jason Junior.
Mahakama ilimpa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa, na shauri hilo limepangwa kuendelea kusikilizwa tena tarehe 02 Juni 2025.