Na WAF, Geneva Uswisi
Prof. Mohammed Janabi, amewasilisha vipaumbele saba ambavyo amevinadi mbele ya Mawaziri wa Afya kutoka nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani katika Bara la Afrika na kuomba ridhaa ya kumpitsha kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani kwa Kanda hiyo.
Prof. Janabi amewasilisha vipaumbele hivyo leo Mei 18, 2025 alipokuwa akijinadi mbele ya Mawaziri hao na kuahidi kuwa endapo atachaguliwa atasimamia uboreshaji wa huduma za afya na kuweka mkazo zaidi kwenye uboreshaji wa huduma za afya ngazi ya msingi.
“Endapo nitachaguliwa naahidi kusimamia uboreshaji wa huduma za afya kwa wote ili kuweza kufikia malengo endelevu,” amesema Prof. Janabi na kuainisha kuwa bado juhudi zinahitajika zaidi kufikia lenngo hilo kwakuwa hadi sasa ni asilimia 46 pekee wanapata huduma bora za afya Barani Afrika huku lengo la kidunia ni kufikia asilimia 68 Mwaka 2030.
Prof. Janabi amesema kuwa atasimamia upatikanaji wa rasilimali fedha za kuwezesha kugharamia upatikanaji wa huduma bora za afya.
Kipaumbele cha tatu amekiainisha kuwa ni kuendelea kusimamia utayari wa nchi wanachama katika kukabiliana na majanga pamoja na dharura za afya.
Prof. Janabi amesisitiza pia kuhusu kuboreha huduma za afya ya uzazi mama na mtoto pamoja na lishe. Amebainisha kuwa Bara la Afrika linachangia asilimia 70 ya vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na asilimia 56 ya vifo vya watoto wachanga duniani.
Kipaumbele cha tano amebainisha kuwa ataendelea kuweka msisitizo zaidi kwenye kupambana na magonjwa ambukizi yakiwemo UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria, Magonjwa yasiyoambukiza pamoja na magonjwa yasiyopewa kipaumbele huku akibainisha kuwa magonjwa yanayotukabili katika bara la afrika yanachangia katika kuzorotesha uchumi wa Bara la Afrika.
Sita, amebainisha kuwa atasimamia jitihada za kupambana na changamoto ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa UVIDA.
“Kuna vifo zaidi ya Milioni 1.2 vinavyotokea Duniani kila mwaka kutokana na UVIDA, bado pia asilimia 40 ya nchi za Afrika hazina mifumo ya usimamizi na udhibiti kukua kwa janga hili,” amesema Prof. Janabi.
Prof. Janabi amehitimsha na kipaumbele cha saba kwa kubainisha kuwa ataimarisha uzalishaji wa bidhaa za afya zikiwemo dawa, vifaa na vifaatiba pamoja na chanjo ndani ya Bara la Afrika.
Prof. Janabi amesema ni muhimu kwa nchi wananchama wa WHO Afrika kuungana pamoja katika kushughulikia changamoto za upatikanaji wa huduma za afya, tafiti na maendeleo ya Sekta ya Afya kwa Bara la Afrika.